पलट जाना

Mkanda wa wampum

Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook kutoka kwa msanii Asili kutoka Amerika Kaskazini ambalo liliondolewa chini ya Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki.

निर्णय का प्रकार

मानक

नीतियां और विषय

विषय
कला / लेखन / काव्य, संस्कृति, अधिकारहीन कम्युनिटी
सामुदायिक मानक
नफ़रत फ़ैलाने वाली भाषा

क्षेत्र/देश

जगह
कनाडा, अमेरिका

प्लैटफ़ॉर्म

प्लैटफ़ॉर्म
Facebook

Muhtasari wa kesi

Dokezo: Mnamo Oktoba 28, 2021, Facebook ilitangaza kwamba ilikuwa ikibadilisha jina la kampuni yake kuwa Meta. Kwenye matini hii, Meta inarejelea kampuni hiyo na Facebook inaendelea kurejelea bidhaa na sera zilizoambatishwa kwenye programu mahususi.

Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook kutoka kwa msanii Asili kutoka Amerika Kaskazini ambalo liliondolewa chini ya Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki. Bodi ilipata kwamba maudhui hayo yapo chini ya mambo yanayoruhusiwa katika sera ya Matamshi ya Chuki kwa kuwa yananuiwa kutoa uhamasisho kuhusu uhalifu wa kihistoria dhidi ya watu Asili ya Amerika Kaskazini.

Kuhusu kesi hii

Mnamo Agosti 2021, mtumiaji wa Facebook alichapisha picha ya mkanda wa wampum, iliyoambatana na maelezo ya maandishi kwa Kiingereza. Mkanda wa wampum ni sanaa Asili ya Amerika Kaskazini ambapo maganda yanafumwa pamoja ili kuunda taswira, kurekodi hadithi na makubaliano. Mkanda huo unajumuisha misururu ya maonyesho ambayo mtumiaji anasema yalitokana na “the Kamloops story,” (hadithi ya Kamloops) rejeleo kwenye ugunduzi wa Mei 2021 wa makaburi yasiyoalamishwa ya shule ya zamani ya makazi ya watoto Asilia wa Uingereza Kolombia, Kanada.

Matini hiyo inatoa kichwa cha kazi hiyo ya sanaa, “Kill the India/Save the Man,” na kutambua mtumiaji kama ndiye muundaji wake. Mtumiaji anaeleza msururu wa taswira zilizoonyeshwa kwenye mkanda huo: “Theft of the Innocent, Evil Posing as Saviours, Residential School / Concentration Camp, Waiting for Discovery, Bring Our Children Home.”(Wizi wa wasio na Hatia, Waovu Wanaojifanya Wakombozi Shule ya Makazi / Kambi ya Utulivu, Kusubiri Kugunduliwa, Leta Watoto Wetu Nyumbani) Kwenye chapisho hilo, mtumiaji anaelezea maana ya kazi yake ya usanii pamoja na historia ya mikanda ya wampum na madhumuni yao kama njia ya elimu. Mtumiaji anataja kwamba ukanda wake haukuwa rahisi kuunda na kwamba iliibua hisia wakati wa kusema hadithi ya kilichofanyika Kamloops. Anaomba radhi kwa maumivu yoyote ambayo kazi hiyo ya usanii ilisababishia manusura wa Kamloops, na kutaja kwamba “madhumuni yake ya kipekee ni kutoa uhamasisho kuhusu hadithi hii ya kutisha.”

Mifumo otomatiki ya Meta ilitambua maudhui hayo kama yanayoweza kukiuka Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki siku iliyofuata baada ya kuchapishwa. Mkaguzi ambaye ni binadamu alitathmini maudhui hayo kama ya ukiukaji na akayaondoa siku iyo hiyo. Mtumiaji alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa Meta na kusababisha ukaguzi wa pili wa binadamu ambao pia ulitathmini maudhui hayo kuwa ya ukiukaji. Kufikia wakati wa kuondolewa kwake, maudhui hayo yalikuwa yametazamwa zaidi ya mara 4,000 na kushirikiwa zaidi ya mara 50. Hakuna watumiaji walioripoti maudhui hayo.

Kutokana na Bodi kuchagua kesi hii, Meta ilitambua kuondolewa kwake kama “utekelezaji wa kimakosa” na ikarejesha maudhui hayo mnamo Agosti 27. Hata hivyo, Meta haikuarifu mtumiaji kuhusu kurejeshwa huko hadi Septemba 30, siku mbili baada ya Bodi kuomba Meta kuipatia maudhui ya ujumbe wake kwa mtumiaji. Meta ilieleza kutoa kwake ujumbe kwa kuchelewa kama kosa la binadamu.

Matokeo muhimu

Meta inakubali kwamba uamuzi wake wa awali wa kuondoa maudhui haya ulikuwa kinyume na Viwango vya Jumuiya ya Facebook na “utekelezaji kimakosa.” Bodi inapata maudhui haya kuwa mfano wazi wa ‘usemi wa makabiliano’ ambapo matamshi ya chuki yanarejelewa ili kupinga udhalimu na ubaguzi.

Utangulizi wa sera ya Facebook ya Usemi wa Chuki inaeleza kwamba usemi wa makabiliano unaruhusiwa pale ambapo nia ya mtumiaji imeonyeshwa wazi. Ni wazi kutoka kwenye maudhui ya chapisho kwamba si matamshi ya chuki. Kazi hiyo ya sanaa inaeleza hadithi ya kilichotokea kule Kamloops, na maneno yanayoambatana nayo yanaeleza umuhimu wake. Ingawa maneno ‘Kill the Indian’ yakiwa pekee yanaweza kuwa ni usemi wa chuki, katika muktadha, kauli hii inavutia makini na kukemea vitendo mahususi vya chuki na ubaguzi.

Bodi inakumbuka uamuzi wake 2020-005-FB-UA katika kesi inayohusisha nukuu kutoka kwa afisa wa Unazi. Kesi hiyo inatoa masomo sawa kuhusu jinsi nia inavyoweza kutathminiwa kupitia viashiria vingine kando na kauli za moja kwa moja, kama vile maudhui na maana ya kauli, muda na nchi ambapo chapisho lilichapishwa, na umuhimu wa hisia na maoni kwenye chapisho hilo.

Katika kesi hii, Bodi ilipata kwamba haikuwa muhimu kwa mtumiaji kutaja moja kwa moja kwamba alikuwa akitoa uhamasisho ndipo chapisho hilo litambulike kama la usemi wa makabiliano. Bodi ilibainisha “Maswali Yanayofahamika” kindani kwa wapatanishi kwamba kutajwa kwa nia kwa uwazi hakutakuwa ni sababu ya kutosha kila mara kubadilisha maana ya chapisho ambalo ni la matamshi ya chuki. Wapatanishi wanatarajiwa kutoa marejeleo kutoka kwa maudhui kutathmini nia, na si kutegemea kauli za moja kwa moja.

Wapatanishi wawili tofauti walihitimisha kwamba chapisho hili lilikuwa la matamshi ya chuki. Meta haikuweza kutoa sababu mahususi za ni kwa nini kosa hili lilitokea mara mbili.

Uamuzi wa Bodi ya Usimamizi

Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa maudhui hayo.

Katika taarifa ya ushauri wa sera, Bodi inapendekeza kwamba Meta:

  • Iwape watumiaji ilani sahihi kwa wakati ufaao kuhusu hatua yoyote ya kampuni inayochukuliwa dhidi ya maudhui ambayo rufaa yao inahusiana nayo. Panapofaa, ikijumuisha katika visa vya makosa ya utekelezaji kama hii, ilani kwa mtumiaji inafaa kukiri kwamba hatua hiyo ilitokana na mchakato wa ukaguzi wa Bodi ya Usimamizi.
  • Italii athari kwa usahihi wa mkaguzi wakati wapatanishi wa maudhui wanapojulishwa kuwa wamehusika katika ukaguzi wa pili, ili wafahamu kwamba uamuzi wa awali ulipingwa.
  • Ifanye tathmini ya usahihi wa mkaguzi inayolenga mambo yanayoruhusiwa katika sera ya Matamshi ya Chuki yanayoshughulikia kujieleza kisanii na kujieleza kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu (m.f., kukemea, kutoa uhamasisho, matumizi ya kujirejelea, matumizi ya uwezeshaji). Tathmini hii pia inapaswa kuchunguza kimahususi jinsi eneo alipo mkaguzi inavyoathiri uwezo wa wapatanishi kutathmini kwa usahihi matamshi ya chuki na usemi wa makabiliano kutoka maeneo sawa au tofauti. Meta inapaswa kushiriki matokeo ya tathmini hii na Bodi, ikijumuisha jinsi matokeo yatakavyosababisha uboreshaji wa utendaji wa utekelezaji na uundaji wa sera na iwapo inapanga kuendesha tathmini za mara kwa mara za usahihi wa mkaguzi kuhusu mambo haya yanayoruhusiwa. Bodi pia inatoa mwito kwa Meta kushiriki kwa umma mihutasari ya matokeo ya tathmini hizi katika visasisho vyake vya uwazi vya kila robo kwa Bodi ili kuonyesha kwamba imetii pendekezo hili.

*Mihtasari ya kesi hutoa maelezo mafupi ya kesi na haina thamani ya kurejelewa katika kesi za baadaye.

Uamuzi kamili wa kesi

1. Muhtasari wa uamuzi

Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa chapisho la msanii Asili wa Amerika Kaskazini ambalo lilijumuisha picha ya sanaa yake pamoja na kichwa chake, ambacho kinanukuu tukio la kihistoria la matamshi ya chuki. Meta ilikubali kwamba chapisho hilo linapatikana katika mambo yanayoruhusiwa ndani ya Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki kwa kuwa ni wazi kwamba nia yake ni kutoa uhamasisho kuhusu uhalifu wa kihistoria dhidi ya watu Asili wa Amerika Kaskazini.

2. Maelezo ya kesi

Mapema Agosti 2021, mtumiaji wa Facebook alichapisha picha ya mkanda wa wampum, iliyoambatana na maelezo ya maandishi kwa Kiingereza. Mkanda wa wampum ni sanaa Asili ya Amerika Kaskazini ambapo maganda yanafumwa pamoja ili kuunda taswira, kurekodi hadithi na makubaliano. Mkanda huo unajumuisha misururu ya maonyesho ambayo mtumiaji anasema yalitokana na “the Kamloops story,” (hadithi ya Kamloops) rejeleo kwenye ugunduzi wa Mei 2021 wa makaburi yasiyoalamishwa ya shule ya zamani ya makazi ya watoto Asilia wa Uingereza Kolombia, Kanada.

Matini hiyo inatoa kichwa cha kazi hiyo ya sanaa, “Kill the India/Save the Man,” na kutambua mtumiaji kama ndiye muundaji wake. Mtumiaji kisha anatoa orodha ya virai vinavyolingana na misururu ya taswira zilizoonyeshwa kwenye mkanda huo: “Theft of the Innocent, Evil Posing as Saviours, Residential School / Concentration Camp, Waiting for Discovery, Bring Our Children Home.”(Wizi wa wasio na Hatia, Waovu Wanaojifanya Wakombozi Shule ya Makazi / Kambi ya Utulivu, Kusubiri Kugunduliwa, Leta Watoto Wetu Nyumbani) Kwenye chapisho hilo, mtumiaji anaelezea maana ya kazi yake ya usanii pamoja na historia ya mikanda ya wampum na madhumuni yao kama njia ya elimu. Mtumiaji anataja kwamba ukanda wake haukuwa rahisi kuunda na kwamba iliibua hisia sana wakati wa kusema hadithi ya kilichofanyika Kamloops. Anaendelea kusema kwamba hadithi hiyo haiwezi kufichwa ili isijulikane kwa umma tena na kwamba anatumai mkanda huo utasaidia kuzuia hiyo kufanyika. Mtumiaji anahitimisha chapisho lake kwa kuomba radhi kwa maumivu yoyote ambayo kazi hiyo ya usanii ilisababishia manusura wa mfumo huo wa shule ya makazi, akisema kwamba “madhumuni yake pekee yalikuwa ni kutoa uhamasisho kuhusu hadithi hii ya kutisha.”

Mifumo otomatiki ya Meta ilitambua maudhui hayo kama yanayoweza kukiuka Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki siku iliyofuata baada ya kuchapishwa. Mkaguzi ambaye ni binadamu alitathmini maudhui hayo kama ya ukiukaji na akayaondoa siku iyo hiyo. Mtumiaji alikata rufaa dhidi ya uamuzi huo kwa Meta na kusababisha ukaguzi wa pili wa binadamu ambao pia ulitathmini maudhui hayo kuwa ya ukiukaji. Kufikia wakati wa kuondolewa kwake, maudhui hayo yalikuwa yametazamwa zaidi ya mara 4,000 na kushirikiwa zaidi ya mara 50. Hakuna watumiaji walioripoti maudhui hayo. Kutokana na Bodi kuchagua kesi hii, Meta ilitambua kuondolewa kwake kama “utekelezaji wa kimakosa” na ikarejesha maudhui hayo mnamo Agosti 27. Hata hivyo, Meta haikuarifu mtumiaji kuhusu kurejeshwa huko hadi Septemba 30, siku mbili baada ya Bodi kuomba Meta kuipatia maudhui ya ujumbe wake kwa mtumiaji. Meta ilieleza kutoa kwake ujumbe kwa kuchelewa kama kosa la binadamu. Ujumbe wenyewe haukumjulisha mtumiaji kwamba maudhui yake yalirejeshwa kama matokeo ya rufaa yake kwa Bodi na Bodi kuteua kesi hii.

Maoni ya umma ya Shirikisho la Masuala ya Mhindi Mmarekani (Maoni ya Umma-10208) yanasema kwamba nukuu hilo lililotumika kama kichwa cha kazi hiyo y sanaa linatoka kwa Richard Henry Pratt, afisa wa jeshi ambaye alifungua shule ya kwanza ya bweni ya shirikisho la Kihindi nchini Marekani. Kirai hicho kilitoa muhtasari wa sera zilizosababisha kuundwa kwa shule za bwei zinazonuia ‘kufanya kuwa wastaarabu’ watu Asili na ‘kuondoa namn zote za utamaduni wa Kihindi.’ Sera sawa na hizo zilitumika nchini Kanada na zimepatikana kusababisha mauaji ya halaiki kitamaduni na Tume ya Ukweli na Maridhiano ya Kanada.

Mtumiaji anaporejelea kilichofanyika “Kamloops”, anarejelea Shule ya Makazi ya Kihindi ya Kamloops, iliyokuwa shule ya bweni ya watoto wa Mataifa ya Kwanza katika Kolombia ya Uingereza, Kanada. Mnamo Mei 2021, viongozi wa Taifa la Kwanza la Tk’emlúps te Secwépemc walitangaza kwamba wamegundua makaburi ambayo hayajaalamishwa kule Kamloops. Mamlaka zimethibitisha maeneo 200 ambayo huenda ni makaburi katika sehemu hiyo.

Serikali ya Kanada inakadiria kwamba idadi ya chini zaidi ya watoto 150,000 asili walipitia mfumo huo wa shule ya makazi kabla ya shule ya mwisho kufungwa mnamo 1997. Watoto asili mara kwa mara walikuwa wakiondolewa katika familia zao kwa nguvu na kuwekewa marufuku ya kujieleza kwa namna yoyote ya utamaduni asili. Shule zilitumia adhabu kali na ya udhalimu na wafanyakazi walijitolea au walivumilia dhuluma za kingono na vurugu mbaya dhidi ya wanafunzi wengi. Wanafunzi walikuwa na utapiamlo, shule hazikuwa na joto na hazikusafishwa ipasavyo, na watoto wengi waliaga kutokana na kifua kikuu na magonjwa mengine bila kupata matibabu ya kutosha. Tume ya Ukweli na Maridhiano ilihitimisha kwamba angalau wanafunzi 4,100 walikufa wakihudhuria shule hizo, wengi kutokana na kutojali kuwahusu au kutelekezwa, namna nyingine kutokana na ugonjwa au ajali.

3. Mamlaka na upeo

Bodi ina mamlaka ya kukagua uamuzi wa Meta kufuatia rufaa kutoka kwa mtumiaji ambaye maudhui yake yaliondolewa (Kifungu cha 2 cha Mkataba, Sehemu ya 1; Sheria ndogo za Kifungu cha 3, Sehemu ya 1). Bodi inaweza kudumisha au kubatilisha uamuzi wa Meta na uamuzi wake una masharti kwa kampuni hiyo (Kifungu cha 4 cha Mkataba). Kifungu cha 3, Sehemu ya 5). Uamuzi wa Facebook unaweza kujumuisha taarifa za ushauri wa sera zenye mapendekezo yasiyo ya kufunga ambayo Meta lazima iyajibu (Kifungu cha 4 cha Mkataba; Kifungu cha 3, Sehemu ya 4).

Bodi inapoteua kesi kama hii, ambapo Meta baadaye inakubali kwamba ilifanya kosa, Bodi hukagua uamuzi wa awali ili kusaidia kuboresha uelewa wa ni kwa nini makosa hutokea, na kufanya mitazamo au mapendekezo yanayoweza kuchangia kupungua kwa makosa na kuboresha mchakato wa kuchunguza ukweli. Baada ya uamuzi wa Bodi katika Dalili za Saratani ya Matiti na Taswira ya Uchi ( 2020-004-IG-UA, Sehemu ya 3), Bodi ilianza kutumia mchakato unaowezesha Meta kutambua makosa yoyote ya utekelezaji kabla ya kesi kukabidhiwa jopo (tazama: ripoti za uwazi, ukurasa wa 30). Si muhimu kwamba katika kesi hizi, Meta inaangazia kigezo chake kikamilifu kwenye uamuzi wake uliopitiwa, kueleza kile ambacho kilifaa kufanyikiamaudhui ya mtumiaji, huku ikiialika Bodi kudumisha hili kama uamuzi wa “mwisho” wa kampuni hiyo. Kando na kueleza ni nini uamuzi ambao mtumiaji alikata rufaa dhidi yake haukuwa sahihi, Bodi ilipendekeza kwamba Meta ieleze jinsi kosa ilivyotokea na kwa nini mchakato wa ndani wa ukaguzi wa kampuni hiyo ilikosa kulitambua au kulisahihisha. Bodi itaendelea kufanya ukaguzi wake kwa mujibu wa uamuzi ambao mtumiaji amekata rufaa dhidi yake.

4. Viwango muhimu

Bodi ya Usimamizi ilizingatia viwango vifuatavyo katika uamuzi wake:

I.Viwango vya Jumuiya ya Facebook:

Viwango vya Jumuiya ya Facebook vinafafanua matamshi ya chuki kama “mashumbulio ya moja kwa moja kwa watu kulingana na kile tunachokiita sifa zilizolindwa — asili ya rangi, kabila, asili ya kitaifa, dini, mwelekeo wa kijinsia, utambulisho wa kijinsia, na ulemavu au ugonjwa hatari.” Chini ya “Ngazi ya 1,” maudhui yaliyopigwa marufuku ni pamoja na “usemi wa vurugu au uungwaji mkono wake kwa maandishi au maonyesho.” Viwango vya Jumuiya pia vinajumuisha mambo yanayoruhusiwa ili kupambanua maudhui yasiyo ya vurugu.

Tunatambua kwamba wakati mwingine watu wanashiriki maudhui ambayo yanajumuisha matamshi ya chuki ya mtu mwingine ili kuyakashifu au kuibua uhamasisho. Katika visa vingine, maneno ambayo yanaweza vinginevyo hukiuka viwango vyetu yanaweza kutumika katika kujirejelea au kwa njia ya uwezeshaji. Sera zetu zimeunda ili kutoa nafasi ya aina hizi za semi, lakini tunawahitaji watu kuashiria kwa wazi lengo lao. Ikiwa lengo halibainishwi, tunaweza kuondoa maudhui.

II. Maadili ya Meta

Maadili ya Meta yameorodheshwa katika utangulizi wa Viwango vya Jumuiya ya Facebook. Maadili ya "Sauti" yametajwa kuwa "muhimu":

Kila mara, lengo la Viwango vyetu vya Jumuiya limekuwa ni kutengeneza mahali pa kujieleza na kuwapa watu sauti. […] Tunataka watu waweze kuzungumza kwa uwazi kuhusu masuala yaliyo muhimu zaidi kwao, hata kama baadhi ya watu wanaweza kutokubaliana nayo au kuona kuwa ni ya kupingwa.

Meta imeweka kikomo cha "Sauti" katika kuhudumia maadili manne na mawili kati ya hayo manne, ni muhimu hapa:

"Usalama". Tumejitolea kufanya Facebook kuwa mahali salama. Kujieleza kwa kutishia watu kuna uwezo wa kuhofisha, kutenga au kunyamazisha wengine na hakukubaliki kwenye Facebook.

“Hadhi”: Tunaamini kwamba watu wote wako sawa kihadhi na kihaki. Tunatarajia kwamba watu wataheshimu hadhi ya wenzao na hawatadhulumu au kuwashusha hadhi.

III. Viwango vya haki za binadamu:

Kanuni za Mwongozo wa Umoja wa Mataifa juu ya Biashara na Haki za Binadamu (UNGP), zilizoidhinishwa na Baraza la Haki za Binadamu la Umoja wa Mataifa mnamo 2011, zina mfumo wa hiari wa majukumu ya haki za binadamu ya biashara za kibinafsi. Mnamo 2021, Meta ilitangazaSera yake ya Haki za Binadamu za Shirika, ambapo ilisisitiza tena kujitolea kwake katika kuwakilisha haki za kibinadamu kwa mujibu wa UNGP. Kigezo ambacho Bodi ilitumia katika kuchambua wajibu wa Meta kwa haki za binadamu katika kesi hii kilitokana na viwango vifuatavyo vya haki za binadamu:

  • Uhuru wa kujieleza: Kifungu cha 19, Agano la Kimataifa kuhusu Haki za Raia na Kisiasa ( ICCPR); Maoni ya Jumla Nambari. 34, Kamati ya Haki za Binadamu, 2011. Kifungu cha 5, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Kuondoa Namna Zote za Ubaguzi wa Rangi ( ICERD); Ripoti ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Matamshi ya Chuki, A/74/486, 2019; Ripoti ya Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu Uratibu wa Maudhui Mtandaoni, A/HRC/38/35, 2018.
  • Usawa na kutobagua: Kifungu cha 2, aya ya. 1 na Kipengele cha 26 (ICCPR); Kifungu cha 2 ICERD; Mapendekezo ya Jumla 35, Kamati ya Uondoaji wa Ubaguzi wa Rangi, 2013.
  • Haki za kitamaduni: Kifungu cha 27 cha ICCPR; Kifungu cha 15, Agano la Kimataifa kuhusu Haki za Kiuchumi, Kijamii na Kitamaduni (ICESCR). Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa katika uwanja wa haki za binadamu, anaripoti kuhusu uhuru wa kisanii na ubunifu, A/HRC/23/34, 2013.
  • Haki za watu asili: Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Asili, Kifungu cha 7, aya ya 2; Kifungu cha 8, aya ya. 1 na Kifungu cha 19 (ICCPR);

5. Taarifa ya mtumiaji

Mtumiaji alisema katika rufaa yake kwa Bodi kwamba chapisho lake lilikuwa likionyesha kipande cha sanaa ya jadi na kuweka kumbukumbu ya historia na kwamba halikuhusiana na matamshi ya chuki kivyovyote. Mtumiaji aliendelea kusema kwamba historia hii “inahitaji kuonekana” na kuhusiana na kuondolewa kwa chapisho hilo na Meta, alisema kwamba “huu ni udhibiti.”

6. Ufafanuzi wa maamuzi ya Meta

Meta iliiambia Bodi kwamba kirai “Kill the Indian” ilikuwa ni sehemu ya shambulio katika Ngazi ya 1 chini ya Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki, ambavyo vinapiga marufuku “usemi wa vurugu” unaolenga watu kwa msingi wa sifa iliyolindwa, ikijumuisha rangi au kabila. Hata hivyo, Meta ilikiri kwamba kuondolewa kwa maudhui hayo kulifanywa kimakosa kwa sababu sera inaruhusu kushiriki matamshi ya chuki ya mtu mwingine ili “kuukashifu au kutoa uhamasisho.” Meta ilibainisha kwamba mtumiaji alitaja katika chapisho kwamba madhumuni yake ilikuwa ni kutoa uhamasisho kuhusu hadithi hiyo ya kutisha kuhusu kile kilichofanyika Kamloops.

Meta ilibainisha kwamba kirai “Kill the Indian/Save the Man” ilitokana na kulazimisha watoto Asili kufanana wa wadhalimu wao. Kwa kutoa uhamasisho kuhusu hadithi ya Kamloops, mtumiaji pia alikuwa akitoa uhamasisho kuhusu kulazimisha watu kufanana kupitia shule za makazi. Katika kujibu swali kutoka kwa Bodi, Meta ilielezea kwamba mkaguzi wa maudhui hangeweza kuwa na ufahamu kuhusu historia hii ndipo atekeleze sera hii kwa usahihi. Chapisho la mtumiaji lilitaja kwamba alikuwa akitoa uhamasisho kuhusu hadithi ya kutisha na hivyo mkaguzi angehitimisha kwamba chapisho hilo lilikuwa likitoa uhamasisho kuhusu matamshi ya chuki yaliyonukuliwa humo.

Meta ilijulisha Bodi kwamba hakuna watumiaji walioripoti maudhui yaliyo kwenye kesi hii. Meta huendesha viainishaji vya mafunzo ya mashine ambavyo vimefunzwa kutambua kiotomatiki ukiukaji unaowezekana wa Viwango vya Jumuiya ya Facebook. Katika kesi hii, vianishaji viwili vilitambua chapisho hilo kiotomatiki kama lenye uwezekano wa kuwa matamshi ya chuki. Kiainishaji cha kwanza, ambacho kilichanganua maudhui hayo, hakikuwa na uhakika sana kwamba chapisho hilo lilikiuka Viwango vya Jumuiya. Hata hivyo, kiainishaji kingine kilipata, kwa msingi wa ishara mbalimbali za kimuktadha, kwamba chapisho hilo linaweza kushirikiwa kwa upana na kuonekana na watu wengi. Kutokana na uwezekano wa madhara yanayoweza kutokea kwa sababu ya kusambaa kwa matamshi ya chuki, mfumo otomatiki wa Meta ulituma chapisho kwa mkaguzi binadamu.

Meta ilieleza katika jibu lake kwa swali la Bodi kwamba mkaguzi binadamu aliye na makao makuu katika eneo la Asia-Pacific alipata kuwa chapisho hilo ni la matamshi ya chuki na akaliondoa kwenye jukwaa. Mtumiaji alikata rufaa na mkaguzi binadamu wa pili aliye katika eneo la Asia-Pacific alihakiki maudhui na pia alipata kwamba lilikuwa ni matamshi ya chuki. Meta ilithibitishia Bodi kwamba wapatanishi hawaweki rekodi ya sababu za maamuzi ya kila maudhui.

7.Mawasilisho ya wahusika wengine

Bodi ya Usimamizi ilizingatia maoni nane ya umma yanayohusiana na kesi hii: manne kutoka Marekani na Kanada, mawili kutoka Ulaya, moja kutoka Kusini Mwa Jangwa la Afrika na moja kutoka Asia-Pacific na Oceania. Mawasilisho hayo yalishughulikia mada zinazojumuisha umuhimu wa nukuu ambalo mtumiaji alitumia kama kichwa cha sanaa yake, muktadha kuhusu matumizi ya shule za makazi katika Amerika Kaskazini na jinsi upatanishi wa maudhui unaofanywa na Meta huathiri uhuru wa kisanii na haki za watu wa utambulisho asili kujieleza huru.

Ili kusoma maoni ya umma yaliyowasilishwa kuhusu kesi hii, tafadhali bofya hapa.

8.Uchambuzi wa Bodi ya Usimamizi

Bodi iliangalia swali la iwapo maudhui haya yanapaswa kurejeshwa kwa Facebook kupitia vigezo vitatu: Viwango vya Jumuiya ya Facebook, maadili ya Meta na wajibu wake kwa haki za binadamu.

8.1 Utiifu wa Viwango vya Jumuiya

Meta ilikubali kwamba uamuzi wake wa awali wa kuondoa maudhui haya ulikuwa kinyume na Viwango vya Jumuiya ya Facebook na ulikuwa “utekelezaji wa kimakosa.” Bodi ilipata kwamba maudhui katika kesi hii si matamshi ya chuki kwa namna isiyo tata. Maudhui haya kuwa mfano wazi wa ‘usemi wa makabiliano’ ambapo matamshi ya chuki yanarejelewa au kuweka upya maana yake ili kupinga udhalimu na ubaguzi.

Viwango vya Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki vinaruhusu moja kwa moja “maudhui ambayo yanajumuisha semi za chuki za mtu mwingine ili kuzikashifu au kutoa uhamasisho.” Wapatanishi wawili tofauti licha ya hayo walihitimisha kwamba chapisho hili lilikuwa la matamshi ya chuki. Meta haikuweza kutoa sababu mahususi za ni kwa nini kosa hili haswa lilitokea mara mbili.

Katika kesi ya Nukuu la Nazi ( 2020-005-FB-UA), Bodi ilibaini kwamba muktadha wa matumizi ya nukuu ni muhimu ili kuelewa maana yake. Katika kesi hiyo, maudhui na maana ya nukuu hiyo, wakati lilichapishwa na nchi ambapo lilichapishwa, pamoja na umuhimu wa hisia na maoni kwenye chapisho hilo, yote yalikuwa yakiashiria wazi kwamba mtumiaji hakunuia kutukuza kitu kilichobainishwa kama chuki.

Bodi imepata kwamba haikuwa muhimu kwa mtumiaji kutaja moja kwa moja kwamba alikuwa akitoa uhamasisho ndipo nia na maana ya chapisho hili liwe wazi. Kazi hiyo ya sanaa iliyo kwenye picha inaeleza hadithi ya kilichotokea kule Kamloops, na maneno yanayoambatana nayo yanaeleza umuhimu wake. Ingawa maneno ‘Kill the Indian’ yakiwa pekee, yanaweza kuwa matamshi ya chuki, kutathmini maudhui hayo kijumla kunafanya kuwa wazi kwamba kauli hiyo imetumika kutoa uhamasisho na kukashifu chuki na ubaguzi. Maudhui yametumika kwenye manukuu ili kupambanua kauli ya chuki na kichwa chake, ambayo kwa kikamilifu yalikuwa “Kill the Indian / Save the Man.” Hii inapaswa kumfanya mkaguzi kusitisha ili kuchunguza kwa kina zaidi. Jinsi mtumiaji alivyosimulia hadithi ya Kamloops na kueleza umuhimu wa kitamaduni wa mkanda wa wampum uliweka wazi kwamba aliwatambua waathiriwa wa ubaguzi na vurugu na si waliofanya vitendo hivyo. Simulizi yake ilikashifu matukio yaliyofichuliwa katika Kamloops kwa uwazi. Ilikuwa wazi kutoka kwenye maoni na hisia kwenye chapisho hilo kwamba nia hii ya kukashifu na kutoa uhamasisho ilieleweka na hadhira ya mtumiaji.

Bodi inasema kwamba “Maswali Yanayofahamika” ya ndani ya Facebook, ambayo ni sehemu ya mwongozo ambao wapatanishi hupewa, yanawaelekeza wapatanishi kutoa makosa upande wa kuondoa maudhui yanayojumuisha matamshi ya chuki pale ambapo nia ya mtumiaji si wazi. Maswali Yanayofahamika pia yanataja kwamba kutajwa kwa nia kwa uwazi hakutakuwa ni sababu ya kutosha kila mara kubadilisha maana ya chapisho ambalo ni la matamshi ya chuki. Mwongozo huu wa ndani unatoa maelekezo yenye kikomo kwa wapatanishi kuhusu jinsi ya kupambanua ipasavyo matamshi ya chuki yaliyopigwa marufuku kutoka kwa usemi wa makabiliano ambao unanukuu matamshi ya chuki ili kuyakashifu au kutoa uhamasisho. Kadri Bodi inavyofahamu, hakuna mwongozo kuhusu jinsi ya kutathmini ushahidi wa nia katika kunukuu maudhui katika muktadha wa kisanii au kutumia maneno ya matamshi ya chuki, au kwenye maudhui yanayojadili ukiukaji wa haki za binadamu, pale ambapo maudhui kama hayo yako chini ya mambo yanayoruhusiwa.

8.2 Utiifu wa maadili ya Meta

Bodi ilipata kwamba uamuzi wake wa awali wa kuondoa maudhui haya uliambatana na maadili ya Meta ya “Sauti” na “Hadhi” na haukuhudumia maadili ya “Usalama.” Ingawa inaambatana na maadili ya Meta ya kuwekea kikomo kuenea kwa matamshi ya chuki kwenye majukwaa yake, Bodi ina wasiwasi kwamba michakato ya upatanishi ya Meta haiwezi kutambua na kulinda uwezo wa watu wanaokabiliwa na utengwaji au ubaguzi kujieleza kupitia usemi wa makabiliano.

Meta imetaja kujitolea kwake kuunga mkono usemi wa makabiliano:

Kama jumuiya, jukwaa la kijamii, na mkutano wa uzoefu wa pamoja wa binadamu, Facebook inaunga mkono mipango ya Usemi wa ukabilianaji kwa kutekeleza sera madhubuti ya maudhui na kufanya kazi pamoja na jamii za ndani, waundaji sera, wataalamu na watengenezaji sera ili kuzindua mipango ya Usemi wa ukabilianaji kote ulimwenguni.

Meta inadai kwamba “Sauti” ndiyo maadili muhimu zaidi ya kampuni hiyo. Sanaa inayolenga kuangazia mambo ya kutisha ya madhila ya kale na kuelimisha watu kuhusu athari zao za kudumu ni mojawapo ya namna muhimu na yenye nguvu zaidi ya kueleza “Sauti,” haswa kwa makundi yaliyotengwa ambao wanaeleza utamaduni wao wenyewe na kujizatiti kuhakikisha kwamba historia yao wenyewe imesikika. Usemi wa makabiliano sio tu namna ya kueleza “Sauti” lakini pia zana muhimu kwa walengwa wa matamshi ya chuki ili kulinda hadhi yao wenyewe na kupambana na unyanyasaji, ubaguzi na mienendo inayoshusha hadhi. Ni lazima Meta ihakikishe kwamba sera zake za maudhui na matendo ya upatanishi yanawajibikia na kulinda namna hii ya kujieleza.

Kwa mtumiaji amaye anatoa uhamasisho kuhusu madhila kwa halaiki kujulishwa kuwa matamshi yake yanagandamizwa kwa kuwa matamshi ya chuki ni kitendo cha kuhujumu hadhi yake. Tuhuma hii, hususan inapothibitishwa na Meta baada ya rufaa, inaweza kusababisha udhibiti binafsi.

8.3 Utiifu wa wajibu wa haki za binadamu wa Meta

Bodi inahitimisha kwamba kuondolewa kwa chapisho hili kulikiuka wajibu wa haki za binadamu wa Meta kama biashara. Meta imeahidi kuheshimu haki za binadamu chini ya Kanuni Zinazoongoza Kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na Haki za Binadamu. ( UNGP). Sera yake ya Haki za Kibinadamu za Shirika inasema kuwa hii inajumuisha Agano la Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR).

Hii ndiyo kesi ya kwanza inayohusu kujieleza kisanii ambayo Bodi imeshughulikia, na vilevile kesi yake ya kwanza inayohusu kujieleza ambapo mtumiaji anajitambulisha kama mtu Asili. Ni mojawapo ya kesi kadhaa ambazo Bodi imeteua ambapo mtumiaji alikuwa akitaka kuvuta makini kwa ukiukaji mbaya wa haki za binadamu.

Uhuru wa kujieleza (Kipengele cha 19 ICCPR)

Viwango vya kimataifa vya haki za binadamu vinasisitiza thamani ya kujieleza kisiasa (Kamati ya Haki za Binadamu Maoni ya Jumla 34, aya ya. 38). Upeo wa ulinzi wa haki hii umebainishwa katika Kifungu cha 19, aya ya 2, ya ICCPR, ambayo inataja kwa njia maalum kauli ya “kwa namna ya sanaa.” Mkataba wa Kimataifa kuhusu Uondoaji wa Aina Zote za Ubaguzi wa Rangi (ICERD), pia unatoa ulinzi dhidi ya ubaguzi katika kutekeleza haki ya uhuru wa kujieleza (Kifungu cha 5), na Kamati iliyo na jukumu la kufuatilia utiifu wa mataifa imesisitiza umuhimu wa haki hiyo kuhusiana na kusaidia "makundi yaliyo hatarini katika kusawazisha uwezo miongoni mwa sehemu za jamii" na ili kutoa "mitazamo mbadala na hoja mbadala" katika majadiliano (Kamati ya CERD, Mapendekezo ya Jumla 35, aya ya 29).

Sanaa mara nyingi huwa ni jambo la kisiasa, na viwango vya kimataifa vinatambua jukumu maalum ya yenye nguvu ya namna hii ya mawasiliano katika hali za kawaida zenye changamoto (Mjumbe Maalum wa Umoja wa Ulaya katika uwanja wa haki za kitamaduni, A/HRC/23/34, aya ya 3 – 4). Intaneti na majukwaa ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook na Instagram haswa, yana thamani maalum kwa wasanii katika kufikia hadhira mpya na pana zaidi. Hali zao za maisha zinaweza kutegemea ufikiaji wa majukwaa ya kijamii yanayotawala Intaneti.

Haki ya uhuru wa kujieleza imehakikishiwa kwa watu wote bila ubaguzi (Kifungu cha 19, aya ya 2, ICCPR). Bodi ilipokea mawasilisho kwamba haki za watu Asili kuwa huru, kabla na baada ya idhini iliyofahamishwa pale ambapo mataifa yanatumia hatua za kisheria au utawala ambazo zinaathiri jumuiya hizo inaashiria kuwajibikia kwa Meta katika kushauriana na jumuiya hizi ikiunda sera zake za maudhui (Maoni ya Umma-10240, Kundi la Haki za Wachache; tazama pia Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Asili, Kifungu cha 19). Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa mawazo na kujieleza ameibua wasiwasi sawa na hiyo katika muktadha wa majukumu ya majukwaa ya mitandao ya kijamii (A/HRC/38/35, aya ya 54).

Maudhui yaliyo katika kesi hii yanahusisha haki zingine kadhaa pia, ikijumuisha haki za watu kutoka miongoni mwa wachache kitaifa, kikabila au kiisimu kufurahia, katika jumuiya iliyo na wengine wa kundi lako, utamaduni wao wenyewe (Kifungu cha 27, ICCPR), na haki ya kushiriki katika maisha ya kitamaduni na kufurahia sanaa (Kifungu cha 15, ICESCR). Sanaa ya kuunda mkanda wa wampum ambayo ililenga kurekodi na kuleta ufahamu wa madhila dhidi ya haki za binadamu na urathi wake unaoendelea inalindwa chini ya Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Watetezi wa Haki za Binadamu, Kifungu cha 6(c), pamoja na haki ya ukweli kuhusu madhila (Seti ya Kanuni za Umoja wa Mataifa za Kukabiliana na Ukiukaji wa Sheria Bila Kuadhibiwa). Azimio la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Watu Asili linatambua kuwa kuondolewa kwa watoto kimabavu kunaweza kuwa kitendo cha vurugu na mauaji ya halaiki (Kifungu cha 7, aya ya 2) na kutoa ulinzi mahususi dhidi ya kufananisha watu kwa kulazimisha na uharibifu wa kitamaduni (Kifungu cha 8, aya ya 1).

Kifungu cha 19 cha ICCPR kinahitaji kwamba pale ambapo serikali imeweka vikwazo dhidi ya semi, vikwazo hivyo lazima vitimize masharti ya kutii sheria, lengo halali na umuhimu na ulinganifu (Kifungu cha 19, aya ya 3 ya ICCPR). Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza amehimiza kampuni za mitandao ya kijamii kuongozwa na kanuni hizi zinapofanya upatanishi mtandaoni, wakikumbuka kwamba udhibiti wa kujieleza kwa kiwango kikubwa na kampuni za kibinafsi kunaweza sababisha wasiwasi haswa katika muktadha huo (A/HRC/38/35, aya za 45 na 70). Bodi imetumia jaribio lenye sehemu tatu kulingana na Kifungu cha 19 cha ICCPR katika maamuzi yake yote hadi kufikia leo.

I. Kutii sheria (uwazi na upatikanaji wa sheria)

Viwango vya Jumuiya kuhusu Usemi wa Chuki vinaruhusu kwa wazi maudhui yanayokashifu matamshi ya chuki au kutoa uhamasisho. Sehemu hii ya sera ni wazi vya kutosha na inaweza kufikiwa na mtumiaji kuelewa kanuni na kutenda ipasavyo (Maoni ya Jumla 34, aya ya 25). Kiwango cha uhalali pia kinahitaji kwamba kanuni zinazobana kujieleza “zitoe mwongozo wa kutosha kwa waliohukumiwa na utekelezaji wao ili kuwawezesha kuwa na uhakika kuhusu aina za usemi zimewekewa kikomo vizuri na aina zisizo na kikomo” (Ibid.) Kukosa kwa wapatanishi hao wawili kutathmini ipasavyo utekelezaji wa mambo yanayoruhusiwa chini ya sera hii kwa maudhui haya kunaashiria kwamba mwongozo zaidi wa ndani kwa wapatanishi unaweza kuhitajika.

II. Lengo halali

Uzuiaji wowote wa jimbo wa uhuru wa kuieleza lazima ufuatilie mojawapo ya malengo halali yaliyoorodheshwa katika Kifungu cha 19, aya ya 3 ya ICCPR. Katika mawasilisho yake kwa Bodi, Meta imekuwa na mtindo wa kuhusisha malengo kutoka kwenye orodha hii kuwa sababu iliyoifanya kugandamiza usemi. Bodi hapo awali ilitambua kwamba Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Matamshi ya Chuki vinafuata lengo halali la kulinda haki za wengine. Haki hizo zinajumuisha haki ya kupata uswa na kutobaguliwa, uhuru wa kujieleza na haki ya uadilifu wa kimwili.

III. Umuhimu na uwiano

Kosa lililo wazi katika kesi hii lina maana kuwa kuondolewa kwake bila shaka hakukuwa muhimu, na Meta imekubali. Bodi ina wasiwasi kwamba kosa kama hilo la utata linaweza kuashiria matatizo makubwa zaidi ya uwiano katika michakato otomatiki na ya ukaguzi wa binadamu ya Meta. Kizuizi chochote cha uhuru wa kujieleza kinapaswa kiwe muhimu ili kufikia utendakazi wake wa ulinzi na kinapaswa kiwe ni chombo cha ukali wa chini zaidi miongoni mwa vile vinavyoweza kufikia utendakazi wao wa ulinzi (Maoni ya Jumla Nambari 34, aya ya 34). Iwapo mifumo ya upatanishi wa maudhui ya Meta inafikia mahitaji ya umuhimu na uwiano inategemea pakubwa ufanisi wake katika kuondoa matamshi halisiya chuki huku ikipunguza idadi ya utambuzi na uondoaji wa kimakosa.

Kila chapisho ambalo limeondolewa kimakosa linahujumu uhuru wa kujieleza. Bodi inaelewa kwamba si rahisi kuepuka makosa, kwa binadamu sawa na mashine. Matamshi ya chuki na majibu kwake yatakuwa katika muktadha mahususi kila mara, na mipaka yake huwa si wazi kila mara. Hata hivyo, aina ya makosa na watu au jumuiya zinazobeba mzigo wa makosa hayo inaakisi uteuzi uliopangwa ambao lazima ufanyiwe tathmini na uchunguzi kila mara. Hii inahitaji uchunguzi zaidi wa sababu kuu za kosa katika kesi hii, na tathmini pana ya jinsi usemi wa makabiliano unavyopatanishwa kwa ufanisi.

Kutokana na umuhimu wa sanaa muhimu kutoka kwa wasanii Asili katika kusaidia kukabiliana na chuki na ugandamizaji, Bodi inatarajia kwamba Meta iwe makini kwa uwezekano wa kuondolewa kwa maudhui kimakosa katika kesi hii na maudhui sawa na hayo kwenye Facebook na Instagram. Haitoshi kutathmini utendaji wa utekelezaji wa sera ya Matamshi ya Chuki ya Facebook unaofanywa na Meta kwa jumla. Mfumo unaofanya vyema kwa wastani unaweza kufanya vibaya katika kategoria ndogo za maudhui ambapo maamuzi yasiyo ya sawa yana athari kubwa kwa haki za binadamu. Inawezekana kwamba aina za makosa ambazo zimetokea katika kesi hii ni nadra. Bodi inabaini, hata hivyo, wanachama wa makundi yaliyotengwa wameibua wasiwasi kuhusu kiwango na athari ya kuondolewa kimakosa kwa miaka kadhaa. Makosa katika kesi hii yanaonyesha kwamba ni jukumu la Meta kuonyesha kwamba imefanya uchunguzi kuhusu haki za binadamu ili kuhakikisha kwamba mifumo yake inafanya kazi kwa usawa na kuendeleza ugandamizaji wa kihistoria na unaendelea (UNGP, Kanuni ya 17).

Meta hutathmini usahihi wa mifumo yake ya utekelezaji kila mara katika kukabiliana na matamshi ya chuki. Utathmini huu haujagawanywa katika tathmini za usahihi ambazo haswa zinakadiria uwezo wa Meta kupambanua matamshi ya chuki kutoka kwa maudhui yanayoruhusiwa yanayokashifu matamshi ya chuki au kutoa uhamasisho.

Michakato iliyopo ya Meta pia inajumuisha mbinu za muda za kutambua mambo yanayovuma kuhusu makosa na kuchunguza sababu zao kuu, lakini hii inahitaji sampuli kubwa za maudhui za kutumika kupima utendaji wa mfumo. Bodi iliuliza iwapo Meta haswa imetathmini utendaji wa mifumo yake ya ukaguzi katika kutathmini kwa usahihi usemi wa makabiliano ambao ni sehemu ya kujieleza kisanii na usemi wa makabiliano kutoa uhamasisho kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu. Meta iliiambia Bodi kwamba haikuwa imefanya utafiti mahususi kuhusu athari ya kuondoa maudhui ya kujieleza kisanii kimakosa au kwenye kujieleza kwa watu wa utambulisho au chimbuko Asili.

Meta imejulisha Bodi kuhusu vizingiti vya kuanza tathmini kama hizo, ikijumuisha ukosefu wa mfumo wa kuweka otomatiki ukusanyaji wa sampuli ya maudhui yanayonufaika kutokana na mambo yanayoruhusiwa katika sera. Hii ilikuwa ni kwa sababu wakaguzi wanatia alama maudhui kuwa ya ukiukaji au yasiyo ya ukiukaji, na hawahitajiki kuashiria ni wapi maudhui yasiyo ya ukiukaji yanahusisha mambo yanayoruhusiwa katika sera. Sampuli ya usemi wa makabiliano ambao unaafiki mambo haya yanayoruhusiwa ingehitajika kukusanywa na mtu mwenyewe.

Ingawa Bodi ilihimizwa na kiwango cha maelezo kilichotolewa kuhusu jinsi Meta inavyotathmini utendaji wakati wa kipindi cha Maswali na Majibu kitakachofanywa kwa ombi la Bodi, ni wazi kwamba uwekezaji zaidi unahitajika katika kutathmini usahihi wa utekelezaji wa sera ya mambo yanayoruhusiwa chini ya Matamshi ya Chuki na kujifunza kutokana na mambo yanayovuma. Bila maelezo ya ziada kuhusu maamuzi ya muundo ya Meta na utendaji wa mifumo yake ya binadamu na otomatiki, ni vigumu kwa Bodi au Meta kutathmini uwiano wa mwelekeo wa sasa wa Meta kwa matamshi ya chuki.

Wakati inapotathmini ikiwa ni muhimu na inawiana kutumia zana za mafunzo ya mashine zinazofanya kazi katika kesi hii kutumbua uwezekano wa kuwepo matamshi ya chuki, kuelewa usahihi wa zana hizo ni muhimu. Vianishaji vya mafunzo ya mashine huhusisha mapishano kati ya viwango vya vitu vinavyoondolewa kimakosa na vitu vinavyoondolewa kwa sawa. Kadri kiainishaji kilivyo makini, ndivyo inavyotambua matukio ya usemi wa chuki, lakini pia uwezekano wa juu wa kualamisha nyenzo zisizo za matamshi ya chuki. Viainishaji vilivyofunzwa tofauti na miundo tofauti inatofautiana kwenye umuhimu na ufanisi wao kwa majukumu tofauti. Kwa muundo wowote ule, upeo tofauti unaweza kutumika unaoakisi uamuzi kuhusu umuhimu linganifu wa kuepuka aina tofauti ya makosa. Uwekezano na kina cha makosa kinapaswa pia kuwa msingi wa maamuzi kuhusu jinsi ya kutumia kiainishaji, ikijumuisha iwapo inaweza kuchukua hatua mara moja au iwapo inahitaji uidhinishaji wa binadamu na ulinzi ambao umewekwa.

Meta ilieleza kwamba chapisho husika katika kesi hii lilitumwa kwa ajili ya ukaguzi na mifumo otomatiki kwa sababu lilikuwa na uwezekano wa kuwa na hadhira kubwa. Mwelekeo huu unaweza kuweka kikomo cha kuenea kwa nyenzo zenye madhara, lakini pia kuna uwezekano wa kuongezeka kwa hatari kwamba sanaa yenye nguvu inayopambana na chuki inaondolewa kimakosa. Meta iliiambia Bodi kwamba inatathmini kiwango cha vitu vinavyoondolewa kimakosa kwa muda, inayopimwa dhidi ya seti ya maamuzi ya wakaguzi wataalamu. Meta pia ilibaini kwamba kuna uwezekano wa kutathmini usahihi wa miundo ya mafunzo ya mashine ambayo ilikuwa muhimu katika kesi hii na kwamba ihifadhi maelezo kuhusu utabiri wa viainishaji vyake kwa angalau siku 90. Bodi iliomba maelezo ambayo yangeturuhusu kutathmini utendaji wa kiainishaji na ufaafu wa upeo ambao Meta ilitumia katika kesi hii. Meta ilijulisha Bodi kwamba haingetoa maelezo ambayo Bodi iliomba kwa sababu haikuwa na muda wa kutosha kuyaandaa kwa ajili yetu. Hata hivyo, Meta ilibaini kwamba ilikuwa ikizingatia uwezekano wa kutoa maelezo haya katika kesi za siku zijazo.

Ukaguzi wa binadamu unaweza kutoa ulinzi mbili muhimu kwa utendaji wa viainishaji vya Meta: kwanza kabla ya chapisho kuondoa na kisha tena baada ya rufaa kukatwa. Makosa katika kesi hii yanaashiria kwamba mwongozo wa Meta kwa wapatanishi unaotathmnini usemi wa makabiliano huenda si toshelevu. Kuna sababu nyingi ambazo huenda zilichangia wapatanishi binadamu kufikia uamuzi usio sahihi mara mbili katika kesi hii. Bodi ina wasiwasi kwamba wakaguzi huenda wasiwe na rasilimali za kutosha kwa namna ya muda au mafunzo ili kuzuia aina ya kosa lililoonekana katika kesi hii, hususan kuhusiana na maudhui yanayoruhusiwa chini ya mambo yanayoruhusiwa katika sera (ikijumuisha, kwa mfano, “kukashifu” matamshi ya chuki na “kutoa uhamasisho”).

Katika kesi hii, wakaguzi walikuwa na makao makuu katika eneo la Asia-Pacific. Meta ilishindwa kujulisha Bodi iwapo viwango vya usahihi wa mkaguzi vilitofautiana kwa wapatanishi wanaotathmini uwezekano wa matamshi ya chuki ambao wapo katika eneo ambapo maudhui hayo yalitoka. Bodi inabaini hali changamano ya kutathmini matamshi ya chuki, na ugumu wa kuelewa muktadha na historia ya ndani, haswa kwa kuzingatia kiwango cha maudhui ambayo wapatanishi hukagua kila siku. Inaweza kueleweka kwamba wapatanishi waliotathmini maudhui katika kesi hii hawakuwa na uzoefu wa kushughulikia ugandamizaji wa watu Asili walio Amerika Kaskazini. Mwongozo unapaswa kujumuisha maelekezo wazi ya kutathmini maudhui kikamilifu na kusaidia wapatanishi katika kutathmini muktadha kwa usahihi zaidi ili kubaini ushahidi wa nia na maana.

Bodi inapendekeza kwenye uamuzi wake wa Meme ya Vitufe Viwili ( 2021-005-FB-UA) kwamba Meta iruhusu watumiaji kuashiria kwenye rufaa yao kwamba maudhui yao yanapatikana miongoni mwa mambo yanayoruhusiwa kwenye Viwango vya Jumuiya ya Facebook kuhusu Usemi wa Chuki. Kwa sasa, mtumiaji anapokata rufaa dhidi ya mojawapo ya uamuzi wa Meta unaoenda kwa mkaguzi binadamu, mkaguzi huyo hajulishwi kwamba mtumiaji amepinga uamuzi uliotangulia na hajui matokeo ya ukaguzi wa uliotangulia. Ingawa Meta imejulisha Bodi kwamba inaamini maelezo haya yataleta upendeleo katika ukaguzi, Bodi ingependa tu kujua iwapo maelezo haya yanaweza kuongeza uwezekano ufanyaji maamuzi kukiwepo tofauti mbalimbali. Hili ni swali ambalo linaweza kujaribiwa kisayansi na Meta; matokeo ya majaribio hayo yanaweza kuwa muhimu katika kutathmini ulinganifu wa hatua mahususi ambazo Meta imeamua kutumia.

Chini ya UNGP, Meta ina wajibu wa kufanya uchunguzi kuhusu haki za binadamu (Kanuni ya 17). Hii inapaswa kujumuisha kutambua athari zozote mbaya za upatanishi wa maudhui kuhusu kujieleza kisanii na kujieleza kisiasa kwa watu Asili wanaokabiliana na ubaguzi. Meta inapaswa kutambua jinsi ya kuzuia, kusuluhisha na kuwajibikia juhudi zake za kushughulikia athari hizo mbaya. Bodi imejitolea kufuatilia utendaji wa Meta na inatarajia kuona kampuni hiyo ikiipa kipaumbele hatari kwa makundi yaliyotengwa na kuonyesha ushahidi wa kuendelea kuboreshwa.

9.Uamuzi wa Bodi ya usimamizi

Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa maudhui hayo.

10. Taarifa ya ushauri wa sera

Utekelezaji

1. Iwape watumiaji ilani sahihi kwa wakati ufaao kuhusu hatua yoyote ya kampuni inayochukuliwa dhidi ya maudhui ambayo rufaa yao inahusiana nayo. Panapofaa, ikijumuisha katika visa vya makosa ya utekelezaji kama hii, ilani kwa mtumiaji inafaa kukiri kwamba hatua hiyo ilitokana na mchakato wa ukaguzi wa Bodi ya Usimamizi. Meta inafaa kushiriki ujumbe wa mtumiaji unaotumwa wakati vitendo vya Bodi vinaathiri maamuzi ya maudhui ambayo watumiaji wamekata rufaa dhidi yake, ili kuonyesha kuwa imetii pendekezo hili. Vitendo hivi vinapaswa kuchukuliwa kuhusiana na kesi zote ambazo zimesahihishwa katika kiwango cha ustahiki cha mchakato wa Bodi.

2. Italii athari ya mielekeo iliyofanyiwa ukarabati kwa ukaguzi wa pili kwa usahihi wa ukaguzi na kote. Haswa, Bodi huomba tathmini ya viwango vya usahihi wapatanishi wa maudhui wanapojulishwa kuwa wamehusika katika ukaguzi wa pili, ili wafahamu kwamba uamuzi wa awali ulipingwa. Jaribio hili linafaa kujumuisha fursa kwa watumiaji kutoa muktadha unaofaa unaoweza kuwasaidia wakaguzi kutathmini maudhui yao, kulingana na mapendekezo ya awali ya Bodi. Meta inafaa kushiriki matokeo ya tathmini hizi za usahihi na Bodi na kutoa mihutasari ya matokeo katika ripoti yake ya uwazi ya kila robo mwaka kwa Bodi ili kuonyesha kwamba imetii pendekezo hili.

3. Ifanye tathmini ya usahihi inayolenga mambo yanayoruhusiwa katika sera ya Matamshi ya Chuki yanayoshughulikia kujieleza kisanii na kujieleza kuhusu ukiukaji wa haki za binadamu (m.f., kukemea, kutoa uhamasisho, matumizi ya kujirejelea, matumizi ya uwezeshaji). Tathmini hii pia inapaswa kuchunguza kimahususi jinsi eneo alipo mkaguzi inavyoathiri uwezo wa wapatanishi kutathmini kwa usahihi matamshi ya chuki na usemi wa makabiliano kutoka maeneo sawa au tofauti. Bodi inaelewa kwamba uchanganuzi huu una uwezekano wa kuhitaji kuundwa kwa sampuli sahihi na zenye lebo zinazofaa za maudhui muhimu. Meta inapaswa kushiriki matokeo ya tathmini hii na Bodi, ikijumuisha jinsi matokeo haya yatakavyosababisha uboreshaji wa utendaji wa utekelezaji na uundaji wa sera na iwapo inapanga kuendesha tathmini za mara kwa mara za usahihi wa mkaguzi kuhusu mambo haya yanayoruhusiwa na kutoa muhtasari wa matokeo katika ripoti yake ya uwazi ya kila robo mwaka kwa Bodi ili kuonyesha kuwa imetii pendekezo hili.

*Dokezo la kiutaratibu:

Maamuzi ya Bodi ya Usimamizi yanatayarishwa na majopo ya Wanachama watano na kuidhinishwa na wengi wa wanachama wa Bodi. Maamuzi ya Bodi hayawakilishi maoni ya kibinafsi ya Wanachama wote.

Kwa uamuzi wa kesi hii, utafiti huru ulipangwa kwa niaba ya Bodi. Taasisi huru ya utafiti yenye makao yake makuu katika Chuo Kikuu cha Gothenburg na iliyotoa timu ya zaidi ya wanasayansi wa kijamii 50 kutoka mabara sita, pamoja na zaidi ya wataalamu 3,200 wa kila nchi kutoka kote ulimwenguni na Washauri kutoka Duco, shirika la ushauri linalolenga mwingiliano wa siasa za dunia, uaminifu na usalama, na teknolojia, walitoa ushauri wa kitaalamu kuhusu muktadha wa jamii na kisiasa na utamaduni.

मामले के निर्णयों और नीति सलाहकार राय पर लौटें