Anulado
Shairi la Kirusi
16 de noviembre de 2022
Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa kwanza wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook linalolinganisha jeshi la Urusi nchini Ukraini na Wanazi na kunukuu shairi linalotaka wafashisti kuuawa
Uamuzi huu unapatikana katika lugha ya Kirusi (kupitia kichupo cha “lugha” kinachofikiwa kupitia menyu iliyo upande wa juu wa skrini hii) katika lugha ya Kilatvia ( hapa) na Kiukraini ( hapa).
Lai iepazītos ar lēmumu latviski, spied šeit.
Щоб прочитати це рішення українською мовою, натисніть тут.
Muhtasari wa kesi
Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa kwanza wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook linalolinganisha jeshi la Urusi nchini Ukraini na Wanazi na kunukuu shairi linalotaka wafashisti kuuawa. Pia imebatilisha ugunduzi wa Meta kwamba picha ya kile kinachoonekana kuwa maiti katika chapisho hilo ilikiuka sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro. Meta ilikuwa imetumia skrini ya onyo kwenye picha hiyo kwa misingi kuwa ilikiuka sera. Kesi hii inaibua baadhi ya masuala muhimu kuhusu uratibu wa maudhui katika hali za migogoro.
Kuhusu kesi hii
Mnamo Aprili 2022, mtumiaji wa Facebook nchini Latvia alichapisha picha ya kile kinachoonekana kuwa maiti, akiangalia chini, barabarani. Hakuna majeraha yanayoonekana. Meta aliithibitishia Bodi kwamba mtu huyo alipigwa risasi huko Bucha, Ukraini.
Maandishi ya Kirusi yanayoambatana na picha hiyo yanasema kwamba maovu yanayodaiwa kufanywa na wanajeshi wa Sovieti nchini Ujerumani katika Vita vya Pili vya Dunia vilisamehewa kwa msingi wa kulipiza kisasi uhalifu ambao askari wa Nazi walikuwa wamefanya huko USSR. Inaleta uhusiano kati ya jeshi la Nazi na jeshi la Urusi huko Ukraini, ikisema jeshi la Urusi “likawa wafashisti.”
Chapisho hilo linataja ukatili unaodaiwa kufanywa na jeshi la Urusi nchini Ukraini na linasema kwamba “baada ya Bucha, Waukrainia pia watataka kurudia... na wataweza kurudia.” Inamalizia kwa kunukuu shairi la “Kill him! (Muue!)” na mshairi wa Soviet Konstantin Simonov, pamoja na mistari: “kill the fascist (Uwa mfashisti)... Kill him! (Muuwe!) Kill him! (Muuwe!) Kill!” (Uwa!)
Chapisho hilo liliripotiwa na mtumiaji mwingine wa Facebook na kuondolewa na Meta kwa kukiuka Viwango vyake vya Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki. Baada ya Bodi kuchagua kesi hiyo, Meta iligundua kuwa imeondoa chapisho hilo kimakosa na kulirejesha. Wiki tatu baadaye, ilitumia skrini ya onyo kwenye picha chini ya sera yake ya Maudhui ya Vurugu na Michoro.
Matokeo muhimu
Bodi imegundua kuwa kuondoa chapisho, na baadaye kutumia skrini ya onyo, hakulingani na Viwango vya Jumuiya ya Facebook, maadili ya Meta, au wajibu wake wa haki za binadamu.
Bodi imegundua kuwa, badala ya kutoa shutuma za jumla kwamba “askari wa Urusi ni Wanazi,” chapisho hilo linasema kuwa walitenda kama Wanazi wakati na mahali mahususi, na husababisha ulinganifu wa kihistoria. Chapisho hilo pia linalenga askari wa Urusi kwa sababu ya jukumu lao kama wapiganaji, sio kwa sababu ya uraia wao. Katika muktadha huu, si wajibu wa Meta wa haki za binadamu wala Kiwango chake cha Jumuiya ya Matamshi ya Chuki inayowalinda wanajeshi dhidi ya madai ya makosa makubwa au kuzuia ulinganisho wa uchochezi kati ya matendo yao na matukio ya zamani.
Bodi inasisitiza umuhimu wa muktadha katika kutathmini iwapo maudhui yanachochea vurugu. Katika kesi hii, Bodi inagundua kwamba nukuu kutoka kwa shairi la “Kill him! (Muuwe!)” ni marejeleo ya kisanii na kitamaduni yanayotumika kama zana ya usemaji. Inaposomwa katika muktadha wa chapisho lote, Bodi inagundua kwamba manukuu yanatumika kuelezea, badala ya kuhimiza, hali ya akili. Yanaonya kuhusu msururu wa matukio ya vurugu na uwezekano wa historia kujirudia nchini Ukraini.
Mwongozo wa ndani wa Meta wa wasimamizi unafafanua kuwa kampuni inatafsiri Viwango vyake vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi ili kuruhusu “marejeleo hayo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea” na “maonyo ya ushauri." Hata hivyo, haijaelezewa katika Viwango vya Jumuiya vya umma. Vivyo hivyo, sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro inakataza picha zinazoonyesha kifo kutokana na vurugu. Mwongozo wa ndani wa wasimamizi unafafanua jinsi Meta huamua kama kifo kinaonekana kuwa kimetokana na vurugu, lakini haijajumuishwa katika sera ya umma.
Katika kesi hii, idadi kubwa ya Bodi inagundua kwamba picha katika chapisho haijumuishi viashiria wazi vya vurugu ambavyo, kulingana na mwongozo wa ndani wa Meta wa wasimamizi, vingehalalisha matumizi ya skrini ya onyo.
Kwa jumla, Bodi imegundua kuwa chapisho hili halina uwezekano wa kuzidisha vurugu. Hata hivyo, inabainisha kwamba kuna matatizo ya ziada ya kutathmini usemi wa vurugu katika hali ya migogoro ya kimataifa ambapo sheria ya kimataifa inaruhusu wapiganaji kulengwa. Uvamizi wa Urusi dhidi Ukraini unatambuliwa kimataifa kuwa ni kinyume cha sheria. Bodi inaitaka Meta kurekebisha sera zake ili kuzingatia mazingira ya kuingilia kijeshi kinyume cha sheria.
Uamuzi wa Bodi ya Usimamizi
Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa kwanza wa Meta wa kuondoa chapisho hilo na uamuzi wake uliofuata kuwa picha kwenye chapisho ilikiuka sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro, na kwa sababu hiyo Meta ilitumia skrini ya onyo.
Bodi inapendekeza kwamba Meta:
- Irekebishe Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi ili kufafanua, kulingana na tafsiri ya Meta ya sera hiyo, kwamba inaruhusu maudhui ambayo yanafanya “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea.”
- Ijumuishe maelezo ya jinsi inavyobainisha ikiwa picha inaonyesha “kifo cha vurugu kwa watu,” katika Viwango vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro.
- Itathmini uwezekano wa kutambulisha zana zinazowaruhusu watumiaji ambao ni watu wazima kuamua kama wataona maudhui ya michoro na, kama wataona, wayaone kwa kutumia skrini ya onyo au bila.
* Mihtasari ya kesi hutoa maelezo mafupi ya kesi na haina thamani ya kurejelewa katika kesi za baadaye.
Uamuzi kamili wa kesi
1. Muhtasari wa uamuzi
Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta kuondoa chapisho la Facebook linalozungumzia mzozo nchini Ukraini. Maudhui, ambayo yapo katika lugha ya Kirusi na yalichapishwa nchini Latvia, yanajumuisha picha yenye mwonekano wa mtaani ya mtu ambaye amelala - anayeweza kuwa amekufa - ardhini, ikiwa imeambatishwa na maandishi. Maandishi hayo yanajumuisha manukuu kutoka kwa shairi maarufu la mshairi wa Kisovieti Konstantin Simonov akitaka upinzani dhidi ya wavamizi wa Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia, na ina maana kwamba wavamizi wa Urusi wana jukumu sawa nchini Ukraini na ambalo wanajeshi wa Ujerumani walikuwa nayo huko USSR. Baada ya Bodi kuchagua chapisho hili ili likaguliwe, Meta ilibadilisha uamuzi wake na ikarejesha maudhui kwenye jukwaa. Maudhui hayo yanaibua maswali muhimu ya ufafanuzi chini ya sera za Meta za Matamshi ya Chuki na Vurugu na Uchochezi. Wiki chache baada ya kuamua kurejesha chapisho hilo, Meta iliweka skrini ya onyo kwenye picha hiyo. Idadi kubwa ya Bodi imegundua kuwa picha hiyo haikiuki sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro, kwa kuwa picha haina viashirio dhahiri vya vurugu, kama ilivyoelezwa katika miongozo ya ndani ya Meta kwa wasimamizi wa maudhui, jambo ambalo linaweza kuhalalisha matumizi ya skrini ya onyo.
2. Maelezo ya kesi na historia
Mnamo Aprili 2022, mtumiaji wa Facebook aliyekuwa nchini Latvia alichapisha picha na matini kwa Kirusi kwenye Mlisho wake. Chapisho hilo lilitazamwa takriban mara 20,000, likashirikiwa takriban mara 100, na likapokea hisia karibu 600 na maoni zaidi ya 100.
Picha hiyo inaonyesha mwonekano wa barabara ambapo mtu amelala, kando ya baiskeli iliyoanguka. Hakuna majeraha yanayoonekana. Maandishi yanaanzia na, “they wanted to repeat and repeated (walitaka kurudia na kurudia.)” Chapisho hilo maoni kuhusu tuhuma za uhalifu uliofanywa na wanajeshi wa Soviet nchini Ujerumani wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Linasema kwamba uhalifu kama huo ulisamehewa kwa msingi kwamba wanajeshi walikuwa wakilipiza kisasi dhidi ya madhila ambayo wana mrengu wa Unazi walifanya dhidi ya muungano wa USSR. Kisha inatoa taswira ya uhusiano kati ya Vita vya Pili vya Dunia na kuvamiwa kwa Ukraini, akihoji kwamba jeshi la Urusi “limekuwa la itikadi ya wafashisti.” Chapisho linasema kwamba jeshi la Urusi nchini Ukraini “rape[s] girls, wound[s] their fathers, torture[s] and kill[s] peaceful people (linabaka wasichana, linawakata kina baba zao, linatesa na kuwauwa watu wenye amani walio katika viunga vya Kyiv vilivyo na amani).” Linahitimisha kwa kusema kwamba “after Bucha, Ukrainians will also want to repeat ... and will be able to repeat” such actions (baada ya Bucha, Wananchi wa Ukraini pia watataka kurudia ... na wataweza kurudia, vitendo kama hivyo).” Mwishoni mwa chapisho hilo, mtumiaji huyo ameshiriki dondoo za shairi “Kill him!”(Muuwe!) la mshairi wa Soviet Konstantin Simonov, ikijumuisha mishororo inayosema: “kill the fascist so he will lie on the ground’s backbone, not you”; “kill at least one of them as soon as you can (muuwe mfashisti ili alale kwenye uti wa mgongo wa ardhi, si wewe”; ua angalau mmoja wao haraka uwezavyo”;) “Kill him! (Muuwe!) Kill him! (Muuwe!) Kill!” (Uwa!)
Siku iyo hiyo maudhui hayo yalichapishwa, mtumiaji mwingine aliyaripoti kama “maudhui ya vurugu na michoro.” Kulingana na uamuzi wa mkaguzi binadamu, Meta iliondoa maudhui hayo kwa kukiuka Viwango vyake vya Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki. Saa chache baadaye, mtumiaji huyo aliyechapisha maudhui hayo alikata rufaa na mkaguzi wa pili alitathmini maudhui hayo kama yanayokiuka sera hiyo.
Mtumiaji alikata rufaa kwa Bodi ya Usimamizi. Kutokana na hatua ya Bodi kuchagua rufaa hiyo ili kufanyiwa ukaguzi mnamo tarehe 31 Mei, 2022, Meta ilibaini kwamba uamuzi wake wa awali wa kuondoa maudhui hayo ulifanywa kimakosa na ikayarejesha. Mnamo Juni 23, 2022, siku 23 baada ya maudhui hayo kurejeshwa, Meta iliweka skrini ya onyo kwenye picha hiyo chini ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro, kwa msingi kwamba inayonyesha kifo cha vurugu cha mtu. Skrini ya onyo inasema “maudhui nyeti – picha hii inaweza kuonyesha maudhui ya vurugu au michoro," na inawapa watumiaji chaguo mbili: “jifunze zaidi” na “tazama picha.”
Historia ifuatayo ya ukweli ni muhimu kwa uamuzi wa Bodi na inategemea utafiti ulioidhinishwa na Bodi:
- Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraini ulitambuliwa kuwa ni kinyume cha sheria na Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa mnamo Machi 2, 2022. ( A/RES/ES-11/1).
- Michelle Bachelet, Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Kibinadamu, alielezea wasiwasi wake wa “maswali muhimu na ya kutatanisha kuhusu uwezekano wa uhalifu wa kivita, ukiukaji mkubwa wa sheria za kimataifa za kibinadamu na ukiukaji mkubwa wa sheria ya kimataifa za haki za binadamu” nchini Ukraini.
- Katika tamaduni za baada ya Soviet, neno “mfashisti” mara nyingi linamaanisha Wanazi wa Ujerumani, haswa katika muktadha wa Vita vya Pili vya Dunia. Hata hivyo, ufafanuzi wa neno “mfashisti” hauhusiani tena moja kwa moja na Wanazi wa Ujerumani. Nchini Urusi na Ukraini, neno hilo liliwekwa ukungu kutokana na mijadala ya kisiasa ambapo neno “mfashisti” limetumika kuwanyanyapaa wapinzani katika sehemu mbalimbali za wigo wa kisiasa.
- “They wanted to repeat and repeated (Walitaka kurudia na wakarudia),” sentensi ya kwanza ya chapisho la mtumiaji, ni rejeleo la “[w]e can repeat (tunaweza kurudia)”, msemo maarufu wa Kirusi, ambao hutumiwa na wengine kurejelea ushindi wa Wasovieti dhidi ya Wanazi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Mtumiaji anataja zaidi msemo huu anaposema kwamba, “baada ya Bucha, Waukrainia pia wanataka kurudia ... na wataweza kurudia” vitendo vya jeshi la Kirusi.
3. Mamlaka na upeo wa Bodi ya Usimamizi
Bodi ina mamlaka ya kukagua uamuzi wa Meta kufuatia rufaa kutoka kwa mtumiaji ambaye maudhui yake yaliondolewa (Kifungu cha 2 cha Mkataba, Sehemu ya 1; Sheria ndogo za Kifungu cha 3, Sehemu ya 1). Bodi inaweza kudumisha au kubatilisha uamuzi wa Meta (Kifungu cha 3, Sehemu ya 5 ya Mkataba), na kampuni itafuata uamuzi huu (Kifungu cha 4 cha Mkataba). Meta pia lazima itathmini uwezekano wa kutekeleza uamuzi wake kuhusiana na maudhui yanayofanana yaliyo katika muktadha tofauti (Kifungu cha 4 cha Mkataba). Uamuzi wa Facebook unaweza kujumuisha taarifa za ushauri wa sera zenye mapendekezo yasiyo ya kufunga ambayo Meta lazima iyajibu (Kifungu cha 3 cha Mkataba, Sehemu ya 4); Kifungu cha 4).
Bodi inapoteua kesi kama hii, ambapo Meta imekubali kwamba ilifanya makosa, Bodi hukagua uamuzi wa awali ili kusaidia kuboresha ufahamu wa ni kwa nini makosa hutokea, na kufanya mitazamo au mapendekezo yanayoweza kuchangia kupunguza makosa na kuboresha taratibu za haki na zenye uwazi.
4. Vyanzo vya mamlaka
Bodi ya Usimamizi ilizingatia mamlaka na viwango vifuatavyo:
I. Maamuzi ya Bodi ya Usimamizi:
Maamuzi muhimu zaidi ya awali ya Bodi ya Usimamizi yanajumuisha:
- Kesi ya “Shirika la Masuala ya Mawasiliano ya Tigray” ( 2022-006-FB-MR). Katika kesi hiyo, Bodi iliunga mkono uamuzi wa Meta wa kuondoa maudhui baada ya kuhitimisha kwamba, kwa kuzingatia wasifu wa mtumiaji (wizara ya serikali ya mkoa), lugha iliyotumika (wito wazi wa kuua askari ambao hawajisalimisha) na ufikiaji wa ukurasa (takriban wafuasi 260,000), kulikuwa na hatari kubwa kwamba chapisho hilo lingeweza kusababisha vurugu zaidi.
- “Kesi ya video ya michoro ya Sudan” ( 2022-002-FB-MR). Katika kesi hii, Bodi ilipendekeza kwamba Meta: (i) irekebishe Kiwango cha Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro ili kuruhusu video za watu au maiti zinaposhirikiwa kwa madhumuni ya kuongeza ufahamu au kuweka kumbukumbu ya ukiukaji wa haki za binadamu; na (ii) kuweka mchakato wa kuunda sera ambao hutengeneza vigezo vya kutambua video za watu au maiti zinaposhirikiwa kwa madhumuni ya kuongeza ufahamu au kuweka kumbukumbu za ukiukaji wa haki za binadamu.
II. Sera za maudhui za Meta:
Chini ya Kiwango cha Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki, Meta hairuhusu matamshi ya “vurugu” au “kudhalilisha” ambayo yanaelekezwa kwa watu au vikundi kwa misingi ya sifa zao zinazolindwa. Sera hiyo inasema kwamba “usemi wa kudhalilisha” inajumuisha “ulinganisho, maelezo ya jumla, au taarifa za tabia isiyokubaliwa kuhusu... wahalifu wa vurugu na wa kingono.” Sera hiyo kwa uwazi haitumiki kwa taarifa za tabia inayokubaliwa. Vikundi vinavyofafanuliwa kuwa “vimetekeleza uhalifu wa vurugu au makosa ya kingono” havilindwi dhidi ya mashambulizi chini ya sera ya Matamshi ya Chuki.
Chini ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi, Meta hairuhusu “vitisho ambavyo vinaweza kusababisha kifo (na aina nyingine za vurugu kali)” ambapo “tishio” linafafanuliwa kama, miongoni mwa mambo mengine, “husababisha vurugu kali” na “taarifa zinazotetea unyanyasaji wa hali ya juu.” Mwongozo wa ndani ya Meta ya wakaguzi wa maudhui unafafanua kuwa kampuni inatafsiri sera hii ili kuruhusu maudhui yaliyo na taarifa yenye “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea ya kitendo au onyo la ushauri.”
Chini ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro, “picha inayoonyesha kifo cha vurugu cha mtu au watu kwa ajali au mauaji” imefunikwa na skrini ya onyo.
III. Maadili ya Meta
Meta imefafanua maadili ya Facebook ya “Sauti,” “Hadhi,” na “Usalama,” miongoni mwa mengine, katika utangulizi wa Viwango vya Jumuiya. Uamuzi huu utarejelea maadili hayo iwapo na kama yanafaa kwa uamuzi.
IV. Viwango vya kimataifa vya haki za binadamu:
Kanuni za Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Binadamu ( UNGP), zilizoidhinishwa na Baraza la Umoja wa Mataifa kuhusu Haki za Binadamu 2011, ziliweka msingi wa utaratibu wa kijitolea wa wajibu wa haki za binadamu wa biashara za kibinafsi. Mnamo 2021, Meta ilitangazaSera yake ya Haki za Binadamu za Shirika, ambapo ilisisitiza tena kujitolea kwake katika kuwakilisha haki za binadamu kwa mujibu wa UNGP. Kigezo ambacho Bodi ilitumia katika kuchambua wajibu wa Meta kwa haki za binadamu katika kesi hii kilitokana na viwango vifuatavyo vya haki za binadamu:
- Haki za uhuru wa kuwa na maoni na kujieleza: Kifungu cha 19, Mkataba wa Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Siasa ( ICCPR), Maoni ya Jumla Nambari. 34, Kamati ya Haki za Binadamu, 2011; Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa maoni na kujieleza, anaripoti: A/HRC/38/35 (2018), A/74/486 (2019) na A/HRC/44/49/Add.2 (2020); Kamishna Mkuu wa Umoja wa Mataifa wa Haki za Binadamu, anaripoti: A/HRC/22/17/Add.4 (2013).
- Usawa na kutobagua: Kifungu cha 2, aya ya 1 (ICCPR).
- Haki ya usalama wa kimwili: Kifungu cha 9 ICCPR.
- Haki ya kuishi: Kifungu cha 6 (ICCPR).
5. Mawasilisho ya mtumiaji
Katika rufaa yake kwa Bodi, mtumiaji anasema kwamba picha aliyoishiriki ndiyo “most innocuous”(haina madhara zaidi) kati ya picha zinazoonyesha hali halisi katika “crimes of the Russian army in the city of Bucha,” (uhalifu wa jeshi la Urusi katika jiji kuu la Bucha,) “where dozens of dead civilians lie on the streets.”(ambapo miili ya maelfu ya raia waliokufa imelala barabarani). Mtumiaji huyo anasema kwamba chapisho lake halitoi mwito wa vurugu na linahusu “past history and the present (historia ya zamani na mambo ya sasa).” Anasema kwamba shairi hilo liliandikwa kulenga “struggle of Soviet soldiers against the Nazis (mapambano ya wanajeshi wa Soviet dhidi ya Wanazi),” na kwamba alilichapisha ili kuonyesha jinsi “the Russian army became an analogue of the fascist army.” (Jeshi la Urusi lilikuwa mfano wa jeshi la wafashisti.) Kama sehemu ya rufaa yake, anasema kwamba yeye ni mwanahabari na anaamini kuwa ni muhimu kwa watu kuelewa kinachofanyika, hususan wakati wa vita.
6. Mawasilisho ya Meta
Katika mantiki ya Meta iliyotolewa kwa Bodi, kampuni ilichanganua maudhui ya kesi hii kwa kuzingatia sera tatu tofauti, kuanzia na Matamshi ya Chuki. Meta iliangazia ni kwa nini kampuni ilibatilisha uamuzi wake wa kwanza, badala ya kueleza jinsi ilivyokuwa imefikia uamuzi wake wa kwanza. Kulingana na Meta, kudai kwamba wanajeshi wa Urusi walifanya uhalifu katika muktadha wa mgogoro wa Urusi na Ukraini hakujumuishi shambulio chini ya sera ya Matamshi ya Chuki kwa sababu “taarifa za tabia zinazokubaliwa” zinaruhusiwa kwenye jukwaa. Meta pia ilieleza kuwa ufashisti ni itikadi ya kisiasa, na kuunganisha tu jeshi la Urusi na itikadi fulani ya kisiasa haimaanishi shambulio kwa sababu “jeshi la Urusi ni taasisi na kwa hivyo sio kikundi cha sifa iliyolindwa au sehemu ndogo inayosimamiwa na sera ya Matamshi ya Chuki (ikilinganishwa na askari wa Urusi, ambao ni watu). Mwishowe, Meta ilionyesha kwamba manukuu tofauti ya shairi la “Kill him! (Muuwe!)” iliyonukuliwa katika maandishi ya chapisho (k.m.,“kill a fascist (uwa Mfashisti),” “kill at least one of them (uwa angalau mmoja wao),” “kill him! (muue!)” yanarejea “Wanazi” katika muktadha wa Vita vya Pili vya Dunia, na Wanazi si kikundi kinacholindwa.
Meta pia ilichambua chapisho hilo kwa kuzingatia sera yake ya Vurugu na Uchochezi. Katika suala hili, Meta ilielezea kwamba “Waukrainia pia watataka kurudia... na wataweza kurudia” baada ya matukio ya Bucha kukosa si utetezi wa vurugu. Meta ilidai kuwa hii ni “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea,” ambayo kampuni inatafsiri kama inaruhusiwa chini ya sera ya Vurugu na Uchochezi. Meta pia ilisema kwamba kunukuu shairi la Simonov ilikuwa njia ya kuongeza ufahamu wa uwezekano wa historia kujirudia nchini Ukraini. Hatimaye, kampuni hiyo ilieleza kuwa kutetea vurugu dhidi ya watu binafsi wanaojumuishwa ndani ya sera ya Watu na Mashirika Hatari, kama vile Wanazi (wanaojulikana kama “Wafashisti” katika shairi la Simonov), kunaruhusiwa chini ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi.
Kisha Meta ilieleza kuwa skrini ya onyo na vizuizi vinavyofaa umri vilitumika kwenye chapisho chini ya sera yake ya Maudhui ya Vurugu na Michoro kwa sababu picha iliyojumuishwa kwenye maudhui inaonyesha kifo cha vurugu cha mtu. Meta ilithibitisha kuwa picha hiyo inaonyesha mtu aliyepigwa risasi huko Bucha, Ukraini.
Kwa kujibu maswali ya Bodi, Meta ilitoa maelezo zaidi ya mipango ambayo imeanzisha katika muktadha wa migogoro nchini Ukraini. Meta ilithibitisha, hata hivyo, kuwa hakuna juhudi zozote kati ya hizi zilizohusika na uondoaji wa mara ya kwanza wa maudhui katika kesi hii au uamuzi wa kuirejesha kwa kutumia skrini ya onyo. Kampuni hiyo iliongeza kuwa imechukua hatua kadhaa kulingana na Kanuni za Mwongozo wa Umoja wa Mataifa kuhusu Biashara na Haki za Kibinadamu ili kuhakikisha uchunguzi unaofaa wakati wa migogoro. Hatua hizi zilijumuisha kuhusika na mashirika ya raia ya Ukrainia na Urusi, na vyombo vya habari huru vya Urusi, kutafuta maoni kuhusu athari za hatua zilizopitishwa na Meta mwanzoni mwa mgogoro.
Bodi iliuliza Meta maswali 11, na Meta ikajibu yote kikamilifu.
7. Maoni ya umma
Bodi ya Usimamizi ilipokea maoni nane ya umma yanayohusiana na kesi hii. Maoni tatu kati ya hayo yaliwasilishwa kutoka Ulaya, nne kutoka Marekani na Kanada, na moja kutoka Marekani Kusini na Karibea. Mawasilisho hayo yalijumuisha mada zifuatazo: migogoro ya kimataifa ya silaha; umuhimu wa muktadha katika udhibiti wa maudhui; jukumu la wanahabari katika hali ya migogoro; nyaraka za uhalifu wa kivita; na usemi wa kisanii.
Ili kusoma maoni ya umma yaliyowasilishwa kuhusu kesi hii, tafadhali bofya hapa.
8. Uchambuzi wa Bodi ya Usimamizi
Hapo awali, Bodi ilikagua ikiwa maudhui yanaruhusiwa chini ya sera za maudhui ya Meta, yanatafasiriwa inapohitajika kulingana na maadili ya jukwaa, na kisha kutathmini kama jinsi maudhui hayo yanavyoshughulikiwa yanalingana na majukumu ya kampuni ya haki za binadamu.
Kesi hii ilichaguliwa na Bodi kwa sababu chapisho hili kuondolewa kuliibua hoja muhimu kuhusu usemi wa kisanii na marejeleo ya kitamaduni yaliyolengwa tena katika miktadha mipya ambayo inaweza kuhatarisha kuchochea vurugu katika hali za migogoro. Mazingira ya mtandaoni za kujieleza ni muhimu hasa kwa watu walioathiriwa na vita na lazima makampuni ya mitandao ya kijamii yazingatie sana kulinda haki zao. Kesi hii inaonyesha jinsi ukosefu wa uchanganuzi wa muktadha, ambao ni wa kawaida katika uratibu wa maudhui kwa kiwango fulani, unaweza kuzuia watumiaji kutoa maoni kuhusu mgogoro, na kusababisha ulinganifu wa kihistoria wa uchochezi.
8.1 Utiifu wa sera za maudhui za Meta
Bodi imegundua kuwa maudhui katika kesi hii hayakiuki Viwango vya Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki, au Kiwango cha Vurugu na Uchochezi. Idadi kubwa ya Bodi imegundua kuwa maudhui hayakiuki Viwango vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro.
I. Matamshi ya Chuki
Sera ya Meta ya Matamshi ya Chuki inakataza mashambulizi dhidi ya watu kwa kuzingatia sifa zinazolindwa, ikiwemo utaifa. Taaluma hupata “ulinzi fulani” inaporejelewa pamoja na sifa inayolindwa. Miongozo ya ndani ya kampuni kwa wasimamizi inafafanua zaidi kwamba “vikundi vidogo vilivyolindwa kwa kiasi fulani,” ikiwemo vikundi vilivyofafanuliwa kwa sifa inayolindwa pamoja na taaluma (k.m., askari wa Urusi), kwa ujumla vina haki ya kulindwa dhidi ya mashambulizi ya Kiwango cha 1 cha Matamshi ya Chuki. Mashambulizi hayo yanajumuisha, miongoni mwa mengine, “usemi wa vurugu” na “usemi wa kudhalilisha... kwa njia ya ulinganisho, maelezo ya jumla, au taarifa za tabia isiyokubaliwa” “kwa au kuhusu... wahalifu wa vurugu na wa kingono.” Sera ya Meta ya Matamshi ya Chuki haitoi ulinzi kwa “vikundi vinavyofafanuliwa kuwa vilitekeleza uhalifu wa vurugu au makosa ya kingono.”
Madai ya kawaida kuwa wanajeshi wa Urusi wanaelekea kutenda uhalifu, yanaweza, kulingana na maudhui na muktadha, kukiuka sera ya Meta ya Matamshi ya Chuki. Madai kama hayo yanaweza kuwa ndani ya kizuizi dhidi ya “usemi wa kudhalilisha” chini ya sera, katika “taarifa za tabia zisizokubalika.” Sera ya Meta inatofautisha kati ya: (i) kikundi kuhusishwa kwa tabia mbaya au sifa zisizofaa kwa sababu ya kabila, asili ya kitaifa au sifa zingine zinazolindwa (hii ndiyo maana ya Meta kwa “kijumla”); (ii) ukosoaji wa wanachama wa kikundi bila muktadha (hii ndiyo maana ya Meta kwa “kauli za kitabia zisizofaa”); na (iii) ukosoaji wa wanachama wa kikundi kwa tabia yao ya zamani (hii ndiyo maana ya Meta kwa :kauli za kitabia zinazofaa”). Katika kesi hiyo, madai kuhusu kuvamia askari wa Urusi yanafanywa katika muktadha wa matendo yao katika mgogoro wa Ukraini, sio kwa ujumla.
Swali hapa ni ikiwa ulinganisho wa mtumiaji wa askari wa Urusi na wafashisti wa Ujerumani wa enzi ya Vita vya Pili vya Ulimwengu, na madai yao kwamba waliwabaka wanawake, waliwaua baba zao, na kuua na kutesa watu wasio na hatia, yalikiuka sera ya Meta ya Matamshi ya Chuki. Meta na Bodi inahitimisha kuwa chapisho hilo halina matamshi ya vurugu au ya kudhalilisha chini ya sera ya Matamshi ya Chuki, ingawa kwa sababu tofauti. Hii ilikuwa sehemu ya pekee ya sera ya Matamshi ya Chuki ambayo imetambuliwa kuwa muhimu katika chapisho hili.
Meta anasema kuwa chapisho hilo halikiuki kwa sababu taarifa za mashtaka zinaelekezwa kwajeshi la Urusi, ambalo ni taasisi, na sio kwa wanajeshi wa Urusi, ambao ni watu. Bodi imegundua kuwa tofauti hii haipo katika kesi hii, kwa kuwa mtumiaji anarejelea “jeshi” na “askari” kwa kubadilishana.
Hata hivyo, Bodi inagundua kwamba mashtaka ya mtumiaji kwamba askari wa Urusi walifanya uhalifu unaoweza kulinganishwa na Wanazi katika muktadha wa uvamizi wa Urusi nchini Ukraini yanaruhusiwa. Ndivyo ilivyo kwa sababu kutaja vitendo maalum (kwa mfano, “walianza kulipiza kisasi – kubaka wasichana, kuwakata baba zao, kuwatesa na kuua watu wenye amani katika sehemu za nje ya Kyiv") na kulinganisha vitendo vya askari wa Urusi nchini Ukraini na vikosi vingine vinavyojulikana kufanya uhalifu wa kivita (k.m., “jeshi la Urusi, baada ya miaka 70, lilijirudia kabisa nchini Ujerumani na [jeshi] la Ujerumani huko Ukraini") ni taarifa “zinazofaa”, zinazohusiana na tabia iliyoonekana wakati wa mgogoro maalum.
Kwa hivyo, Bodi inagundua kwamba kulinganisha vitendo vya askari wa Urusi katika muktadha mahususi na uhalifu wa Wanazi kunaruhusiwa chini ya Viwango vya Jumuiya, licha ya iwapo ulinganisho wa jumla na Wanazi unaruhusiwa au la. Kulingana na miongozo ya ndani ya Meta, nyenzo ambazo zinaweza kujumuisha matamshi ya chuki hazikiuki sera hiyo ikiwa zinalengwa dhidi ya vikundi “vinavyofafanuliwa kuwa vilitekeleza uhalifu wa vurugu au makosa ya kingono.” Kwa upana zaidi, haikiuki sera ya matamshi ya chuki ya kuripoti matukio ya ukiukaji wa haki za binadamu katika muktadha mahususi, hata kama watu hao wanatambuliwa kwa kurejelea asili yao ya kitaifa.
Bodi pia inagundua kwamba madondoo tofauti ya shairi la “Kill him! (Muuwe!)” iliyonukuliwa katika maudhui (k.m., “kill a fascist (Uwa mfashisti),” “kill at least one of them (uwa angalau mmoja wao),” “kill him! (muuwe!)” haipaswi kuzingatiwa kuwa “usemi wa vurugu” kwa sababu, inaposomwa pamoja na sehemu nyingine ya chapisho hilo, Bodi inaelewa kuwa mtumiaji anatoa mwito kuhusu msururu wa matukio ya vurugu, badala ya kuhimiza vurugu.
Hatimaye, Bodi inahitimisha kuwa wanajeshi wa Urusi wanalengwa katika chapisho hilo kwa sababu ya jukumu lao kama wapiganaji, na wala sio utaifa wao. Madai hayo si mashambulizi yanayoelekezwa kwa kikundi “kwa msingi” wa sifa zao zinazolindwa. Inafuata kwamba maudhui sio matamshi ya chuki, kwa sababu hakuna tabia inayolindwa inayohusika.
II. Vurugu na Uchochezi
Chini ya sera ya Vurugu na Uchochezi, Meta huondoa “wito wa vurugu kali,” "taarifa zinazotetea vurugu kali,” na “taarifa za matamanio au zenye masharti ya kufanya vurugu kali,” miongoni mwa aina nyingine za usemi. Miongozo ya ndani ya kampuni kwa wasimamizi unafafanua zaidi kwamba Meta inatafsiri Kiwango hiki cha Jumuiya ili kuruhusu taarifa zenye “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea ya kitendo au onyo la ushauri.” Zaidi ya hayo, miongozo ya ndani inaeleza “maudhui ambayo yanashutumu au kuongeza ufahamu wa vitisho vya vurugu” pia yanaruhusiwa chini ya sera ya Vurugu na Uchochezi. Hii inatumika kwa maudhui ambayo “yanataka kufahamisha na kuwaelimisha wengine kwa uwazi kuhusu mada au suala fulani; au maudhui yanayozungumzia uzoefu wa mtu kuwa mlengwa wa tishio au vurugu,” ikiwemo ripoti za kitaaluma na midia.
Meta iliieleza Bodi kuwa iliamua kurejesha maudhui haya kwa sababu chapisho hilo halikutetea vurugu. Meta inabainisha taarifa ya mtumiaji kwamba “Ukrainians will also want to repeat … and will be able to repeat (Wakrainia pia watataka kurudia ... na wataweza kurudia)” baada ya matukio huko Bucha kama “maejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea,” ambayo kampuni inatafsiri kama inaruhusiwa chini ya sera ya Vurugu na Uchochezi. Meta pia inasma kwamba kunukuu shairi la Simonov ilikuwa njia ya kuongeza ufahamu wa uwezekano wa historia kujirudia yenyewe nchini Ukrainia. Mwishowe, ikionyesha ukweli kwamba shairi la Simonov linaelekezwa dhidi ya mafashisti wa Ujerumani, inabainisha kuwa kutetea vurugu dhidi ya watu waliojumuishwa katika sera ya Watu na Mashirika Hatari, kama Wanazi, inaruhusiwa chini ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi.
Bodi imeshawishika kwa kiasi fulani na hoja hii. Inakubali kwamba sentensi “Ukrainians will also want to repeat... and will be able to repeat (Waukrainia pia watataka kurudia ... na wataweza kurudia)” haitoi wito wala kutetea vurugu. Kusoma neno kwa neno, sehemu hii ya chapisho inasema tu kwamba Waukrainia wanaweza kujibu kwa ukali vitendo vya jeshi la Urusi kama vile Wasovieti walivyofanya kwa Wanazi. Kwa maneno mengine, ni “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea,” yanayoruhusiwa kulingana na tafsiri ya Meta ya sera ya Vurugu na Uchochezi, iliyobainishwa katika miongozo ya ndani inayotolewa kwa wasimamizi wa maudhui.
Bodi pia inagundua kuwa madondoo yenye lugha ya vurugu ya shairi la “Kill him! (Muuwe!)” iliyotajwa katika sehemu iliyo hapa juu, inaweza kusomwa kama inayoelezea, sio kutia moyo, hali ya akili. Inaposomwa pamoja na chapisho lote, ikiwemo picha, dondoo ni sehemu ya ujumbe mpana wa onyo la uwezekano wa historia kujirudia nchini Ukraini. Ni marejeleo ya kisanii na kitamaduni ambayo hutumiwa kama zana ya usemaji na mtumiaji ili kuwasilisha ujumbe wao. Kwa hivyo, Bodi inahitimisha kwamba sehemu hii ya maudhui pia inaruhusiwa na miongozo ya ndani ya Meta.
Bodi inahitimisha, hata hivyo, kwamba Meta haina uhalisia inapochanganua chapisho hilo kana kwamba ni mwito tu wa vurugu dhidi ya Wanazi. Mtumiaji anaweka wazi kuwa anachukulia wanajeshi wa Urusi nchini Ukraine leo kama Wajerumani nchini Urusi wakati wa Vita vya Pili vya Dunia. Kwa kiwango ambacho chapisho hilo, pamoja na manukuu yake kutoka kwa shairi la Simonov, linaweza kuzingatiwa kuwa linarejelea askari ambao sasa wanafanya maovu dhidi ya raia, kuna hatari kwamba wasomaji watasoma hii kama mwito wa vurugu dhidi ya askari wa Urusi leo. Hata hivyo bodi inakubaliana na hitimisho la Meta kwamba chapisho halikiuki Kiwango cha Vurugu na Uchochezi kwa sababu maana yake msingi, katika muktadha, ni onyo dhidi ya marudio ya vurugu.
III. Maudhui ya Vurugu na Michoro
Chini ya sera yake ya Maudhui ya Vurugu na Michoro, Meta huongeza lebo za maonyo kwenye maudhui “ili watu watambue hali ya picha au michoro kabla ya kubofya ili kuiona.” Hivyo ndivyo ilivyo kwa “Taswira zinazoonyesha kifo cha mtu kupitia vurugu au cha watu kupitia ajali au mauaji.” Katika miongozo yake ya ndani kwa wasimamizi wa maudhui, Meta inafafanua kama “viashiria vya kifo cha vurugu” taswira ya “baada ya kifo cha vurugu ambapo mwathiriwa anaonekana amekufa au hajiwezi, na kuna viashirio vya ziada vya vurugu,” kama vile “damu au majeraha mwilini, damu inayomzunguka mwathiriwa, mwili uliovimba au uliobadilika rangi, au miili iliyochimbwa kutoka kwa uchafu.” Miongozo ya ndani inaeleza zaidi kwamba miili isiyo na “kiashirio chochote kinachoonekana cha kifo cha vurugu” au bila “angalau kiashirio kimoja cha vurugu” haipaswi kuchukuliwa kuwa onyesho la “kifo cha vurugu.”
Picha iliyojumuishwa kwenye maudhui inaonyesha mwonekano wa barabara na mtu ambaye amelala tuli chini. Hakuna majeraha yanayoonekana. Meta iliweza kuthibitishwa kwamba mtu huyo alipigwa risasi huko Bucha, Ukraini. Bodi inabainisha kuwa wasimamizi wa maudhui wanaofanya kazi kwa kiwango fulani si lazima wapate ufikiaji wa aina hii ya maelezo. Idadi kubwa ya Bodi imegundua kuwa sera ya Maudhui ya Virugu na Michoro haikukiukwa kwa sababu picha haina viashirio dhahiri vya vurugu, kama ilivyoelezwa katika miongozo ya ndani ya Meta kwa wasimamizi wa maudhui. Kwa hivyo, wengi wanahitimisha kuwa skrini ya onyo haikufaa kutumika.
Kwa kuzingatia muktadha wa migogoro ya silaha nchini Ukrainia na uchafu ulioonyeshwa kwenye picha, wachache kwenye Bodi wamegundua kwamba maudhui hayakiuki sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro.
IV. Hatua ya utekelezaji
Maudhui hayo yaliripotiwa na mtumiaji chini ya Maudhui ya Vurugu na Michoro lakini yaliondolewa chini ya sera ya Matamshi ya Chuki. Ilirejeshwa tu baada ya kuzingatiwa na Bodi. Katika kujibu maswali kutoka kwa Bodi, Meta ilieleza kuwa maudhui ya kesi hayakutumwa kwa wataalamu wa sera au mada kwa ajili ya ukaguzi wa ziada. “Imetumwa ili ikaguliwe” inamaanisha kuwa, badala ya uamuzi kuangaliwa upya na wasimamizi wa maudhui wanaofanya ukaguzi wa kiwango fulani, inatumwa kwa timu ya ndani ya Meta ambayo inawajibika kwa sera au eneo husika.
8.2 Utiifu wa maadili ya Meta
Bodi imegundua kuwa kuondoa maudhui na kuweka skrini ya onyo juu ya picha iliyojumuishwa, hakulingani na maadili ya Meta.
Bodi ina wasiwasi kuhusu hali ya raia wa Urusi, na athari zinazoweza kutokea za usemi wa vurugu yanayolenga Warusi kwa jumla. Hata hivyo, katika kesi hii, Bodi imegundua kuwa maudhui hayasababishi hatari kwa “Hadhi” na “Usalama” wa watu hao ambao wanaweza kuhalalisha kuondoa “Sauti,” hasa katika hali ambayo Meta inapaswa kuhakikisha kuwa watumiaji walioathiriwa na vita kuweza kujadili athari zake.
8.3 Utiifu wa wajibu wa haki za binadamu wa Meta
Bodi imegundua kuwa uamuzi wa kwanza wa Meta wa kuondoa maudhui na uamuzi wa Meta wa kutumia skrini ya onyo kwenye maudhui yote hayakuwa yanalingana na majukumu ya Meta ya haki za binadamu kama biashara. Meta imeahidi kuheshimu haki za binadamu chini ya Kanuni Zinazoongoza Kanuni za Umoja wa Mataifa kuhusu biashara na Haki za Binadamu. ( UNGP). Sera ya Facebook ya Haki za Kibinadamu za Shirika inasema kuwa hii inajumuisha Agano la Kimataifa kuhusu Haki za Kiraia na Kisiasa ( ICCPR).
Uhuru wa kujieleza (Kifungu cha 19 ICCPR)
Upeo wa haki ya uhuru wa kujieleza ni mpana. Kifungu cha 19, aya ya 2, ya ICCPR inatoa ulinzi wa hali ya juu kwa usemi, ikiwemo usemi wa kisanii, kuhusu masuala ya kisiasa, na maoni kuhusu masuala ya umma, pamoja na mijadala ya haki za binadamu na madai ya kihistoria ( Maoni ya Jumla Nambari 34, aya ya 11 na 49). Hata usemi ambao unaweza kuchukuliwa kuwa ya “kuchukiza sana” una haki ya kulindwa (Maoni ya Jumla Nambari 34, aya ya 11). Maudhui yanayochanganuliwa na Bodi katika kesi hii yana maneno makali. Hata hivyo, ni sawa na mazungumzo ya kisiasa na yanaonyesha haki za binadamu katika muktadha wa vita.
Maudhui katika kesi hii yalijumuisha manukuu kutoka kwa shairi maarufu la vita, ambalo mtumiaji alilitumia kama marejeleo ya kitamaduni ya uchochezi ili kujulisha na kuonya hadhira yao kuhusu madhara yanayoweza kusababishwa na vitendo vya wanajeshi wa Urusi nchini Ukraini. Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza amesisitiza kwamba usemi wa kisanii unajumuisha “hadithi za kubuni na zisizo za kubuni ambazo huelimisha au kugeuza au kuchochea” ( A/HRC/44/49/Add.2, aya ya 5).
Kifungu cha 19 cha ICCPR kinahitaji kwamba pale ambapo serikali imeweka vikwazo dhidi ya semi, vikwazo hivyo lazima vitimize masharti ya kutii sheria, lengo halali, na umuhimu na ulinganifu (Kifungu cha 19, aya ya 3 ya ICCPR). Mjumbe Maalum wa Umoja wa Mataifa kuhusu uhuru wa kujieleza amehimiza makampuni ya mitandao ya kijamii kuongozwa na kanuni hizi wakati wa kudhibiti kujieleza mtandaoni ( A/HRC/38/35, aya ya 45 na 70).
I. Kutii sheria (uwazi na upatikanaji wa sheria)
Kanuni ya uhalali inahitaji kanuni zinazotumika na majimbo kuzuia usemi ili uwe unaoeleweka na unaoweza kufikiwa (Maoni ya Jumla ya 34, aya ya 25). Kamati ya Haki za Binadamu imeendelea kusema kwamba kanuni “haziwezi kuwapa usiri usiozuiwa kwa vikwazo vya uhuru wa kujieleza kwa wale waliopewa jukumu la utekelezaji wake” (Maoni ya Jumla 34, aya ya 25. Watu binafsi lazima wawe na maelezo ya kutosha ili kubaini ikiwa na jinsi kujieleza kwako kunaweza kuwekewa kikomo, ili waweze kurekebisha mienendo yao ipasavyo. Inatumika kwa sheria za maudhui za Meta kwa Facebook, watumiaji wanapaswa kuelewa kinachoruhusiwa na kilichopigwa marufuku.
Sehemu mbili kutoka kwa miongozo ya ndani ya Meta kuhusu jinsi ya kutekeleza Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi ni muhimu hasa kwa hitimisho lililofikiwa na Meta na Bodi kwamba maudhui yanapaswa kusalia kwenye Facebook. Kwanza, Meta inatafsiri sera hii ili kuruhusu ujumbe ambao unaonya kuhusu uwezekano wa vurugu kutoka kwa wahusika wengine, ikiwa ni taarifa zenye “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea ya kitendo au onyo la ushauri.” Pili, vinginevyo kukiuka maudhui kunaruhusiwa ikiwa “inashutumu au kuongeza ufahamu wa vitisho vya vurugu.” Bodi inabainisha, hata hivyo, kuwa miongozo hii ya ndani haijajumuishwa katika lugha inayoonekana hadharani ya Viwango vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi. Hii inaweza kusababisha watumiaji kuamini kuwa maudhui kama vile chapisho katika kesi hii yanakiuka, kumbe hayajakiuka. Meta inapaswa kujumuisha sehemu hizi katika lugha inayoonekana hadharani ya sera ya Vurugu na Uchochezi, ili iwe wazi kabisa kwa watumiaji. Bodi inafahamu kwamba kutangaza maelezo zaidi kuhusu sera za maudhui ya Meta kunaweza kuwawezesha watumiaji wenye nia mbaya kukiuka Viwango vya Jumuiya kwa urahisi. Bodi inazingatia, hata hivyo, kwamba hitaji la uwazi na hali maalum linatumika kwa wasiwasi kwamba baadhi ya watumiaji wanaweza kujaribu “kuchanganya mfumo.” Kutojua kuwa kuruhusu “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo ya matokeo yanayoweza kutokea,” “maonyo ya ushauri,” “kushutumu” au “kuongeza ufahamu” kuhusu vitisho vya vurugu kunaweza kusababisha watumiaji kuepuka kuanzisha au kujihusisha katika mijadala ya mapendeleo ya umma kwenye majukwaa ya Meta.
Bodi pia ina wasiwasi kwamba katika kesi hii, uamuzi wa Meta wa kuweka skrini ya onyo haulingani na miongozo yake ya ndani kwa wasimamizi wa maudhui. Zaidi ya hayo, huenda tafsiri ya Meta kuhusu sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro inaweza sio wazi kwa watumiaji. Meta inapaswa kutaka kufafanua, katika lugha ya sera inayoonekana hadharani, jinsi kampuni inavyotafsiri sera hiyo, na jinsi inavyobainisha ikiwa taswira “inaonyesha kifo cha vurugu cha mtu au watu kwa ajali au mauaji,” katika muktadha wa migogoro, kulingana na miongozo ya ndani ya Meta kwa wasimamizi wa maudhui.
Zaidi ya hayo, Meta iliarifu Bodi kuwa hakuna ujumbe uliotumwa kwa mtumiaji ambaye aliripoti maudhui ili kuwajulisha kuwa chapisho hilo lilirejeshwa baadaye na kampuni hiyo. Hii inazua maswala ya uhalali, kwani watumiaji kukosa kupata maelezo muhimu huenda ukaingilia “uwezo wa mtu binafsi wa kupinga vitendo vya maudhui au kufuatilia malalamiko yanayohusiana na maudhui” ( A/HCR/38/35, katika aya 58). Bodi inabainisha kuwa kuwafahamisha wanahabari kuhusu hatua ya utekelezaji iliyochukuliwa dhidi ya maudhui waliyoripoti, na Kiwango cha Jumuiya husika kinachotekelezwa, kungesaidia watumiaji kuelewa na kufuata vyema sheria za Meta.
II. Lengo halali
Kikwazo chochote dhidi ya uhuru wa kujieleza kinapaswa pia kufuata “lengo halali.” Hapo awali Bodi ilitambua kuwa Viwango vya Jumuiya kuhusu Matamshi ya Chuki kinafuata lengo halali la kulinda haki za watu wengine (Maoni ya Jumla Nambari 34, aya ya 28), ikijumuisha haki za usawa na kutobaguliwa kwa misingi ya kabila na asili ya kitaifa (Kifungu. 2, aya ya 1, ICCPR). Kuwalinda Warusi wanaolengwa na chuki, kwa hviyo, ni lengo halali. Hata hivyo, Bodi inagundua kuwa kuwalinda “askari” kutokana na madai ya kutenda makosa sio lengo halali, wanapolengwa kwa sababu ya jukumu lao kama wapiganaji wakati wa vita, sio kwa sababu ya utaifa wao au sifa nyingine iliyolindwa; ukosoaji wa taasisi kama vile jeshi haupaswi kupigwa marufuku (Maoni ya Jumla Nambari 34, aya ya 38).
Kiwango cha Vurugu na Uchochezi, ambacho kimewekwa na kutumiwa ipasavyo, hufuata lengo halali la kulinda haki za wengine. Katika muktadha wa kesi hii, sera hii inalenga kuzuia ghasia kuongezeka ambayo inaweza kusababisha madhara kwa usalama wa kimwili (Kifungu cha 9, ICCPR) na maisha (Kifungu cha 6, ICCPR) ya watu katika maeneo yaliyoathiriwa na mgogoro Urusi na Ukrainia.
Bodi inabainisha kuwa kuna matatizo ya ziada yanayohusika katika kutathmini usemi wa vurugu katika muktadha waupinzani wa kutumia silaha dhidi ya uvamizi. Uvamizi wa Urusi dhidi ya Ukraini unatambuliwa kimataifa kuwa ni kinyume cha sheria (A/RES/ES-11/1), na matumizi ya nguvu ili kujilinda dhidi ya vitendo hivyo vya uchokozi inaruhusiwa (Kifungu cha 51, Mkataba wa Umoja wa Mataifa). Katika muktadha wa migogoro ya kimataifa ya silaha, sheria ya kimataifa ya kibinadamu kuhusu mwenendo wa wahusika kwenye mapigano inaruhusu wapiganaji walio hai kulengwa kihalali wakati wa mapigano ya silaha. Hivi sivyo ilivyo kwa watu kutoshiriki tena kikamilifu katika uhasama, wakiwemo wafungwa wa vita (Kifungu cha 3, Mkutano wa Geneva unaohusiana na Utendeaji wa Wafungwa wa Vita). Ambapo unyanyasaji yenyewe ni halali chini ya sheria ya kimataifa, matamshi yanayohimiza vurugu kama hiyo inatoa mambo tofauti ambayo lazima yachunguzwe tofauti. Ingawa Bodi imegundua maudhui katika kesi hii kuwa hayakiuki, Bodi inaitaka Meta kurekebisha sera zake ili kuzingatia hali ya kuingilia kijeshi kinyume cha sheria.
Kwa kurejelea uamuzi wa kampuni wa kuweka skrini ya onyo kwenye picha hiyo, Meta inabainisha kuwa sera ya maudhui ya Vurugu na Michoro inalenga kukuza mazingira ambayo yanafaa kwa ushiriki wa aina mbalimbali kwa kuweka vizuizi kwa “maudhui yanayosifu vurugu au kusherehekea mateso au fedheha ya wengine.” Bodi inakubali kwamba lengo hili ni halali katika muktadha wa lengo la Meta la kukuza jukwaa linalojumuisha wote.
III. Umuhimu na uwiano
Kanuni ya umuhimu na usawa inatoa vizuizi vyovyote vya uhuru wa kujieleza “lazima viwe vinafaa ili kufanikisha kazi yao ya ulinzi; lazima viwe ni vyombo vya ukali wa chini zaidi kati ya vile vinavyoweza kufikia lengo lao la ulinzi; [na] lazima viwe na usawa na mapendeleo ya kulindwa” (Maoni ya Jumla ya 34 aya ya 34).
Ili kutathmini hatari zinazoletwa na maudhui ya vurugu au chuki, Bodi kwa kawaida huongozwa na jaribio la vipengele sita lililofafanuliwa katika Mpango wa Utekelezaji wa Rabat, ambalo hushughulikia utetezi wa chuki ya kitaifa, mbari au kidini unaojumuisha uchochezi wa uhasama, ubaguzi au vurugu. Katika kesi hii, Bodi inagundua kuwa, licha ya muktadha wa migogoro ya silaha inayoendelea na marejeleo ya kitamaduni yanayoshtakiwa ambayo yalitumiwa na mtumiaji, kuna uwezekano kwamba chapishovonyo dhidi ya marudio ya vurugu – litasababisha madhara. Bodi inahitimisha kuwa uondoaji wa maudhui mara ya kwanza haukuwa muhimu. Zaidi ya hayo, idadi kubwa ya Bodi inagundua kwamba skrini ya onyo pia haikuwa ya lazima, ilhali idadi ndogo ya Bodi wanagundua kuwa ilikuwa muhimu na sawia.
Kwa kuzingatia mambo yanayohusika hapa, Bodi inahitimisha kuwa licha ya muktadha wa uvamizi haramu wa Urusi dhidi ya Ukrainia ambapo matamshi yanayoweza kuwa ya uchochezi yanaweza kuongeza mgogoro, nia dhahiri ya mtumiaji (kuongeza ufahamu kuhusu vita na matokeo yake), ufafanuzi uliotumika katika kunukuu shairi la vita, na mawasiliano mengine yanayoenea kuhusu matukio ya kutisha nchini Ukrainia, inamaanisha kuwa maudhui hayawezi kuchangia pakubwa katika kuzidisha vurugu.
Idadi kubwa ya Bodi huhitimisha kuwa matumizi ya skrini ya onyo huzuia uhuru wa kujieleza na sio jibu la lazima katika tukio hili, kwa kuwa picha haina viashirio dhahiri vya vurugu, kama ilivyoelezwa katika miongozo ya ndani ya Meta kwa wasimamizi wa maudhui, jambo ambalo linaweza kuhalalisha matumizi ya skrini ya onyo. Makampuni ya mitandao ya kijamii yanapaswa kuzingatia aina mbalimbali za majibu yanayowezekana kwa maudhui yenye matatizo ili kuhakikisha kuwa vizuizi vinapunguzwa ( A/74/486, aya ya 51). Kwa hivyo, Bodi inazingatia kwamba Meta inapaswa kuendeleza zaidi zana za kugeuza kukufaa ili watumiaji waweze kuamua iwapo wataona maudhui nyeti ya michoro wakitumia maonyo au bila maonyo kwenye Facebook na Instagram.
Idadi chache ya Bodi wanaona kuwa skrini ya onyo ilikuwa hatua muhimu na yenye usawa ambayo iliundwa ipasavyo ili kuhimiza ushiriki na uhuru wa kujieleza. Idadi ngogo wanaamini kwamba, kwa kuzingatia utu wa watu waliofariki, haswa katika muktadha wa mapigano ya silaha, na athari zinazowezekana za picha zinazoonyesha kifo na vurugu kwa idadi kubwa ya watumiaji, Meta inaweza kukosea kwa kuongeza skrini za onyo juu ya maudhui sawa na yanayochanganuliwa.
9. Uamuzi wa Bodi ya usimamizi
Bodi ya Usimamizi imebatilisha uamuzi wa kwanza wa Meta wa kuondoa maudhui, na uamuzi uliofuata wa Meta kwamba sera ya Maudhui ya Vurugu na Michoro ilikiukwa, hali iliyosababisha kampuni kuweka skrini ya onyo kwenye picha katika chapisho.
10. Taarifa ya ushauri wa sera
Sera ya maudhui
1. Meta inapaswa kuongeza kwa lugha inayoonekana hadharani ya Viwango vyake vya Jumuiya kuhusu Vurugu na Uchochezi kwamba kampuni inatafsiri sera ili kuruhusu maudhui yaliyo na taarifa zenye “marejeleo yasiyokuwa na upendeleo kwa matokeo yanayoweza kutokea ya kitendo au onyo la ushauri,” na maudhui “yanayoshutumu au huongeza ufahamu wa vitisho vya vurugu.” Bodi inatarajia kuwa pendekezo hili, likitekelezwa, litahitaji Meta kusasisha lugha inayoonekana hadharani ya sera ya Vurugu na Uchochezi ili kuakisi ujumuishaji huu.
2. Meta inapaswa kuongeza kwa lugha inayoonekana hadharani ya Viwango vyake vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro, maelezo kutoka kwa miongozo yake ya ndani kuhusu jinsi kampuni inavyoamua ikiwa picha “inaonyesha kifo cha vurugu cha mtu au watu kwa ajali au mauaji.” Bodi inatarajia kwamba pendekezo hili, likitekelezwa, litahitaji Meta kusasisha lugha inayoonekana hadharani Viwango vya Jumuiya kuhusu Maudhui ya Vurugu na Michoro ili kuakisi ujumuishaji huu.
Utekelezaji
3. Meta inapaswa kutathmini uwezekano wa kutekeleza zana za kugeuza kukufaa ambazo zingeruhusu watumiaji wenye umri wa zaidi ya miaka 18 kuamua kama wataona maudhui nyeti ya michoro wakitumia skrini za onyo au bila, kwenye Facebook na Instagram. Bodi inatarajia kwamba pendekezo hili, likitekelezwa, litahitaji Meta kuchapisha matokeo ya tathmini ya uwezekano.
*Dokezo la kiutaratibu:
Maamuzi ya Bodi ya Usimamizi yanatayarishwa na majopo ya Wanachama watano na kuidhinishwa na wengi wa wanachama wa Bodi. Maamuzi ya Bodi hayawakilishi maoni ya kibinafsi ya Wanachama wote.
Kwa uamuzi wa kesi hii, utafiti huru ulipangwa kwa niaba ya Bodi. Taasisi huru ya utafiti yenye makao yake makuu katika Chuo Kikuu cha Gothenburg na iliyotoa timu ya zaidi ya wanasayansi wa kijamii 50 kutoka mabara sita, pamoja na zaidi ya wataalamu 3,200 wa kila nchi kutoka kote ulimwenguni. Bodi pia ilisaidiwa na Duco Advisors, shirika la ushauri linalolenga miingiliano ya siasa za ulimwengu, uaminifu na usalama na teknolojia. Kampuni ya Lionbridge Technologies, LLC, ambayo wataalamu wake wanajua lugha zaidi ya 350 na hufanya kazi kutoka miji 5,000 ulimwenguni kote, ilitoa utaalamu wa kiisimu.
Volver a Decisiones de casos y opiniones consultivas sobre políticas