أسقط
Kiongozi mpinzani wa ukoloni Amílcar Cabral
تم النشر بتاريخ 27 حَزِيران 2023
Mtumiaji alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook lililohusisha shairi linalorejelea kiongozi wa Ginebisau ambaye ni mpinzani wa utawala wa ukoloni Amílcar Cabral. Baada ya Bodi kuifahamisha Meta kuhusu rufaa hiyo, kampuni hiyo ilibatilisha uamuzi wake wa awali na ikarejesha chapisho hilo.
Huu ni uamuzi kwa ufupi.Uamuzi wa ufupi huchunguza kesi ambapo Meta ilibatilisha uamuzi wake wa kwanza kuhusu kipande cha maudhui baada ya Bodi kupeleka kesi hiyo kwa kampuni. Uamuzi huu unajumuisha maelezo kuhusu makosa ambayo Meta ilikiri. Huidhinishwa na jopo la Wanachama wa Bodi, si Bodi kamili. Huwa hauzingatii maoni ya umma wala hauna thamani ya kutumiwa kama marejeleo kwa Bodi. Uamuzi kwa ufupi hutoa uwazi kuhusu masahihisho ya Meta na kuangazia sehemu zenye uwezekano wa kuboreshwa katika utekelezaji wa sera zake.
Muhtasari wa kesi
Mtumiaji alikata rufaa dhidi ya uamuzi wa Meta wa kuondoa chapisho la Facebook lililohusisha shairi linalorejelea kiongozi wa Ginebisau ambaye ni mpinzani wa utawala wa ukoloni Amílcar Cabral. Baada ya Bodi kuifahamisha Meta kuhusu rufaa hiyo, kampuni hiyo ilibatilisha uamuzi wake wa awali na ikarejesha chapisho hilo.
Maelezo na historia ya kesi
Mnamo Januari 2023, mtumiaji wa Facebook alichapisha maudhui kwa Kifaransa ili kuadhimisha kifo cha Amílcar Cabral katika siku ya maadhimisho ya kuuawa kwake mwaka wa 1973. Cabral ana umaarufu kote ulimwenguni kama mwenye fikra za Uafrika ambaye hatimaye alifanikiwa kuongoza vuguvugu la kuleta mageuzi dhidi ya utawala wa kikoloni wa Ureno nchini Ginebisau na Kepuvede. Chapisho hilo lilikuwa na shairi, linalosifu michango ya Cabral katika harakati za kupambana na ukoloni na athari yake katika bara zima la Afrika. Mtumiaji alidai kuwa shairi hilo liliandikwa mwaka 1973 na kuchapishwa katika jarida la African-Asian.
Meta awali iliondoa chapisho hilo kwenye Facebook, ikitaja sera yake ya Watu na Mashirika Hatari (DOI), ambayo chini yake, kampuni hiyo huondoa maudhui “yanayosifu,” “kuunga mkono pakubwa,” au “kuwakilisha” watu na mashirika ambayo kampuni hiyo imebainisha kuwa ni hatari.
Katika rufaa yake kwa Bodi, mtumiaji huyo alisema kwamba shairi hili limekuwepo kwa miongo mingi na lilichapishwa ili kumuenzi Amílcar Cabral.
Baada ya Bodi kuwasilisha kesi hii kwa Meta, kampuni hiyo ilibaini kuwa uamuzi wake wa kuondoa maudhui hayo haukuwa sahihi na ikarejesha maudhui hayo kwenye jukwaa hilo. Kampuni hiyo iliiambia Bodi kwamba kiongozi huyo wa Ginebisau, Amílcar Cabral hajabainishwa kama mtu hatari katika sera yake ya DOI lakini anaweza kuhusishwa kimakosa na mtu mwingine ambaye amebainishwa. Chapisho hilo kurejea mauaji ya 1973 kunaashiria hadhira ambayo mchapishaji alilenga. Kutokana na ukaguzi wake katika kesi hii, Meta ilisema kuwa iliboresha desturi zake za utekelezaji “ili kuepuka uondoaji wa maudhui kwa ukweli ambao si hasa kwa kusifu mtu ambaye hajabainishwa kama mtu hatari, Amílcar Cabral.”
Mamlaka na upeo wa Bodi
Bodi ina mamlaka ya kukagua uamuzi wa Meta kufuatia rufaa kutoka kwa mtumiaji ambaye maudhui yake yaliondolewa (Kifungu cha 2 cha Mkataba, Sehemu ya 1; Sheria ndogo za Kifungu cha 3, Sehemu ya 1).
Pale ambapo Meta inakiri kwamba ilikosea na ibatilishe uamuzi wake katika kesi inayoshughulikiwa ili ikaguliwe na Bodi, Bodi inaweza kuchagua kesi hiyo ili kuifanyia uamuzi kwa ufupi (Sheria ndogo Kifungu cha 2, Sehemu ya 2.1.3). Bodi hupitia uamuzi wa kwanza ili kuongeza uelewa wa mchakato wa uratibu wa maudhui, ili kupunguza makosa na kuongeza haki kwa watu wanaotumia Facebook na Instagram.
Umuhimu wa kesi
Kesi hii inaangazia kosa ambalo linaweza kutokea katika utekelezaji wa sera ya Meta ya DOI. Katika uamuzi nne wa awali, Bodi imetoa mapendekezo 13 mahususi ikirai Meta kueleza wazi sera hii na utekelezaji wake (“ Kutajwa kwa neno Taliban katika kuripoti habari,” mnamo Septemba 2022, “ Chapisho la Al Jazeera lililoshirikiwa” mnamo Septemba 2021, “ Kutengwa kwa Öcalan” mnamo Julai 2021, na “ Nukuu ya Nazi” Januari 2021). Meta imetekeleza au kuripoti kupiga hatua katika mapendekezo hayo 10, huku ikikataa kutekeleza mapendekezo matatu. Hatua zaidi ikipigwa na Meta katika kusasisha sera yake ya DOI na kuboresha mifumo husiani ya uratibu inaweza kusaidia kupunguza viwango vya makosa katika uratibu wa maudhui.
Katika kesi ya Amílcar Cabral, Bodi iliiomba Meta kusasisha desturi zake za utekelezaji ili kuepuka kuondoa maudhui yanayomtaja kimakosa, hali itakayotumika kote kwenye jukwaa hili kwa machapisho sawa na hili.
Uamuzi
Bodi imebatilisha uamuzi wa awali wa Meta wa kuondoa maudhui hayo. Bodi inatambua masahihisho ambayo Meta ilifanya kwenye kosa la kwanza baada ya Bodi kujulisha Meta kuhusu kesi hiyo.
العودة إلى قرارات الحالة والآراء الاستشارية المتعلقة بالسياسة